Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Machar: Siko tayari kurejea nchini Sudan Kusini kwa sasa

April 19, 2019

Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar amesema hayuko tayari kurejea nchini mwake kwa sasa, huku akitoa mwito wa kuahirishwa mchakato wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

 

Puot Kang Chol, msemaji wa chama cha SPLM-IO cha Riek Machar amesema kiongozi huyo wa upinzani hayuko tayari kurejea nchini Sudan Kusini kwa sasa, na angependa mpango huo wa kurejea nchini kwa lengo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa uahirishwe kwa muda wa miezi sita au zaidi.

 

Amebainisha kuwa, Machar hawezi kurejea Juba bila kudhaminiwa usalama wake, huku akikanusha madai kuwa wanajeshi wapatao 3,000 wa serikali na upinzani wanafanya mazoezi ya pamoja, ikiwa ni sehemu ya mkakati huo wa kuunda serikali jumuishi.

 Machar alitazamiwa kurejea nchini Sudan Kusini mwezi ujao wa Mei, chini ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa baina yake na Rais Salvaa Kiir mwezi Septemba mwaka jana huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, kwenda kuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

 Alhamisi ya wiki iliyopita, mahasimu hao wawili wa kisiasa wa Sudan Kusini walikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mwezi Septemba mwaka jana, katika mkutano wa Vatican, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki mjini Rome, Italia

 

Nchi ya Sudan Kusini iliyojitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani, Disemba mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi

 

www.mzunguko.com

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload