Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Rwanda yawaenzi waliouawa katika mauaji ya kimbari robo karne iliyopita

April 7, 2019

Wananchi wa Rwanda leo wamekusanyika kuwaenzi Watutsi 800,000 na Wahutu wenye misimamo ya wastani waliouawa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyojiri katika kipindi cha miezi mitatu miaka 25 iliyopita.

 

Hafla hiyo ya leo ni mwanzo wa shughuli ya wiki nzima ya kuwaenzi waliouawa katika mauaji hayo yaliyoishtua dunia. Rais Paul Kagame wa Rwanda ameweka shada la maua eneo la Gisozi palipo kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ambapo watu karibu robo milioni wamezikwa.

 

Viongozi wa nchi 10 wameshiriki katika shughuli hiyo akiwemo Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker na marais wa nchi kadhaa za Kiafrika.

 

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalijiri kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvanal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali. SHambulizi hilo lilipelekea wanajeshi wa Kihutu serikali na wanamgambo waitifaki waliokuwa na misimamo mikali kuanzisha mauaji ya kimbari kwa lengo la kuwaangamiza Watutsi waliokuwa wachache.

 

Wakati huo huo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameipatia kamisheni moja ya nchi hiyo jukumu la kufuatilia iwapo Paris ilikuwa na nafasi katika mauaji ya halaiki ya muongo wa 90 nchini Rwanda .

 

Kabla ya hapo pia rais wa zamani wa Ufaransa, François Hollande alijaribu kufichua nyaraka za kihistoria zinazohusiana na jinai hiyo, ingawa baadaye watafiti walidai kwamba Hollande hakutumia vyanzo vya kiutaalamu katika uwanja huo.

 

www.mzunguko.com

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload