Polisi: Gaidi aliyeua msikitini New Zealand kukabiliwa na mashitaka 50 ya mauaji


Polisi ya New Zealand imesema gaidi kwa jina Brenton Tarrant raia wa Australia ambaye alihusika katika shambulizi dhidi ya msikiti mmoja kati ya miwili iliyoshambuliwa nchini New Zealand mnamo Machi 15 atapandishwa kizimbani kesho Ijumaa, akikabiliwa na mashitaka 50 ya mauaji na 39 ya jaribio la mauaji

Taarifa iliyotolewa na Polisi ya New Zealand imesema Tarrant mwenye umri wa miaka 28 atapandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya mji wa Christchurch kupitia njia ya video.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, waendesha mashitaka wangali wanatathmini iwapo gaidi huyo ataongezewa mashitaka mbali na 89 yanayomuandama, chini ya sheria mpya ya kupambana na ugaidi nchini humo.

Jaji wa Mahakama Kuu nchini New Zealand, Cameron Mander amesema kikao cha kesho cha kusikiliza mashitaka yanayomkabili gaidi huyo kitakuwa cha urasimu tu, na kwamba mshitakiwa hatahitajika kukubali au kukanusha mashitaka dhidi yake.

Katika shambulio hilo la Ijumaa ya Machi 15, kijana huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu ambaye alitangaza mwenyewe kuwa mfuasi wa Rais Donald Trump wa Marekani aliyarusha hewani mubashara mauaji hayo ya kinyama aliyoyafanya katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.

Watu wasiopungua 50 wakiwemo wanawake na watoto wadogo waliuawa na makumi ya wengine walijeruhiwa katika mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya misikiti miwili katika mji wa Christchurch nchini New Zealand wakati waumini wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya Sala ya Ijumaa.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu