Philip Hammond: Kujiuzulu Theresa May hakutasaidia kutatuliwa kadhia ya Brexit

March 24, 2019

Waziri wa Fedha wa Uingereza Philip Hammond ametoa tamko kufuatia kuenea habari kwamba huwenda Theresa May, Waziri Mkuu wa nchi hiyo akajiuzulu nafasi yake na kusema kuwa, mabadiliko ya serikali nchini hayawezi kusaidia kutatua kadhia ya Brexit.

 

 

Hammond ameongeza kwamba, Waingereza lazima wafuate njia iliyoratibiwa kwa ajili ya kuiondoa nchi yao katika Umoja wa Ulaya, na si kushinikiza kujiuzulu  kwa Theresa May.

 

Akizungumzia taarifa zilizoenezwa na vyombo vya habari kuhusiana na juhudi za baadhi ya mawaziri kwa ajili ya kumsambaratisha waziri mkuu huyo mwanamke Philip Hammond amesema kuwa,

 

suala hilo halina ukweli na kusisitiza kwamba kumuingiza madarakani waziri mkuu mpya hakuwezi kusaidia utatuzi wa mgogoro huo.

 

Inafaa kuashiria kwamba gazeti la kila wiki la The Sunday Times limeandika kwamba, jumla ya mawaziri 11 wa serikali ya Uingereza wanaendesha mchakato wa kumshinikiza Theresa May ajiuzulu nafasi yake..

Philip Hammond, Waziri wa Fedha wa Uingereza.

 

Kwa mujibu wa habari hiyo, mchakato huo utakamilika hivi karibuni sana na kwamba ndani ya kipindi cha siku 10, May atakuwa ameng'atuka madarakani.

 

Aidha gazeti hilo limebainisha kwamba, kuna uwezekano nafasi ya May ikashikiliwa kwa muda na David Lidington, Naibu Waziri Mkuu, ingawa pia limetaja majina ya Michael Gove, Waziri wa Mazingira, na Jeremy Hunt, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo. 

 

Wabunge wa Uingereza itawapasa wapige kura ya ama kujitoa katika Umoja wa Ulaya ifikapo Aprili 12 na wala sio Machi 29 kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali, au kuchelewesha mchakato huo.

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumapili ya jana mamia ya maelfu ya wananchi wa Uingereza walifanya maandamano  makubwa katika mji mkuu London, kushinikiza kufanyika kura mpya ya maoni kuhusu suala la kujitoa kwa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya (Brexit).

 

www.mzunguko.com

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon