Makumi ya wanahabari waandamana Sudan kulalamikia ukandamizaji wa al-Bashir

March 24, 2019

Makumi ya wanahabari wameandamana leo katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum wakitaka kuachiliwa huru Osman Mirghani, Mhariri Mkuu wa gazeti mashuhuri la al-Tayar na kulalamikia ukandamizaji wa vyombo vya usalama dhidi ya waandamanaji.

 

Mhariri huyo alitiwa mbaroni mwezi uliopita muda mchache baada ya kufanya mahojiano na televisheni ya Sky News na kukosoa vikali hatua ya Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo ya kutangaza hali ya hatari.

 

Waandishi hao wa habari leo waliandamana kuonyesha mshikamano wao na Osman Mirghani ambaye angali anashikiliwa na vyombo vya usalama vya Sudan.

 

Wakiwa wamebeba mabango na maberamu wanahabari hao wametangaza kuwa, wao ni sauti ya wananchi na kwamba, wanataka Mirghani aachiliwe huru.

 

Tangu katikati ya mwezi Desemba mwaka jana hadi sasa, Sudan imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi na ongezeko la bei za bidhaa.

Maandamano ya wananchi wa Sudan dhidi ya Rais Omar al-Bashir

 

Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

 

Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha yamebadilika na kuwa wimbi la kumtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia uongozini.

 

Makumi ya waandamanaji ambao wanataka Rais Omar al-Bashir ang'atuke madarakani wametiwa mbaroni, huku ripoti za asasi za kiraia zikieleza kuwa watu zaidi ya watu 50 wameuawa hadi sasa katika ghasia na machafuko huko Sudan.

 

Licha ya kutangazwa hali ya hatari na hata kuundwa baraza jipya la mawaziri, yote hayo hayajafanikiwa kutuliza hali ya mambo kwani maandamano hayo yameendelea kushuhudiwa karibu kila siku nchini Sudan.

 

www.mzunguko.com

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon