Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Watu zaidi ya 130 wauawa Mali, UN yashtushwa na mauaji hayo

March 24, 2019

Watu zaidi ya 130 wameuawa baada ya wavamizi waliobeba silaha kushambulia kijiji cha watu wa kabila la Fulani katika eneo la Ogossagou katikati mwa Mali.

 

Kwa mujibu wa Boubacar Kane, Gavana wa wilaya ya Bankass, wawindaji wa kabila la Dogon ndio waliofanya hujuma hiyo dhidi ya jamii ya Fulani jana Jumamosi.

 

Mashuhuda wanasema wavamizi hao wameteketeza karibu nyumba zote zilizokuwa kwenye kijiji hicho.

Mauaji hayo yamefanyika katika hali ambayo, ujumbe wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa umeitembelea nchi hiyo ya Kiafrika inayoshuhudiwa mapigano na mauaji ya mara kwa mara.

 

Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres amesema, "Katibu Mkuu ameshtushwa na kusikitishwa na mauaji hayo ya raia 134 wakiwemo watoto wadogo na wanawake. Vyombo vya dola nchini Mali vichunguze mauaji hayo na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wake."

Amesema Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA kinafanya operesheni ya angani ili kuzuia mauaji mengine ya aina hiyo, sanjari na kusaidia kuwahamisha majeruhi.

 

Mapema mwaka huu,  watu wengine 37 wa kabila la Fulani waliuawa katika mapigano ya kikabila katika eneo la Mopti nchini Mali.

 

Mapigano ya kikabila nchini Mali haswa baina ya kabila la kuhamahama la Tuareg na lile la wafugaji la Fulani hadi hivi sasa yameshaua mamia ya watu na kupelekea makumi ya maelfu ya wengine kukimbia makazi yao.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload