Magaidi kadhaa wa Daesh wauawa na maafisa usalama wa Tunisia


Maafisa usalama wa Tunisia wamefanikiwa kuwaangamiza wanachama watatu wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

Kanali Houssem Jbebli, afisa usalama katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Maafisa wetu wa usalama wameua watu watatu wanaosadikiwa kuwa wanamgambo wa Daesh baada ya kupambana vikali katika milima ya Saloum katika eneo la Kasserine."

Hata hivyo hajaeleza iwapo maafisa usalama wa Tunisia waliuawa au kujeruhiwa katika mapigano hayo ya jana Jumanne.

Siku chache kabla ya makabiliano hayo ya jana, genge hilo la kigaidi lilichapisha picha zinazowaonesha wanachama wa kundi hilo wakitembea huku wamebeba silaha walizokuwa wamezificha kwenye eneo hilo la milima.

Tunisia inakumbwa na wimbi la mashambulizi ya kigaidi baada ya kutokea mapinduzi ya wananchi mwaka 2011, yaliyomuondoa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zine Abidine Ben Ali.

Tangu tarehe 24 Novemba 2015 baada ya kutokea shambulio la kigaidi la Daesh dhidi ya basi moja la askari wa ulinzi wa Rais mjini Tunis, ambapo watu 38 waliuawa wakiwemo maafisa 12 wa polisi, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inatekeleza sheria ya hali hatari.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu