Taarifa za visanduku vyeusi: Ajali ya ndege ya Ethiopia 'inafanana' na ya Lion Air ya Indone


Taarifa za awali zilizopatikana kwenye vinasa taarifa na sauti vya ndege ya Ethiopia iliyoanguka siku kadhaa zilizopita zinaonyesha kuwa, kuna "mshabihiano wa wazi" kati ya ajali ya ndege hiyo na ile ya shirika la ndege la Indonesia la Lion Air iliyotokea mwezi Oktoba mwaka jana.

Waziri wa Usafiri wa Ethiopia Dagmawit Moges amewaeleza waandishi wa habari kuwa, kisanduku cheusi kimepatikana kikiwa katika hali nzuri kuwezesha kupata taarifa karibu zote zilizomo ndani yake.

Bi Moges ameongeza kuwa, taarifa hizo zitasaidia katika uchunguzi zaidi utakaofanywa kuhusu chanzo cha ajali hiyo, huku ripoti yake ya awali ikitazamiwa kutolewa ndani ya siku 30 zijazo.

Waziri wa Usafiri wa Ethiopia, Dagmawit Moges akizungumza na waandishi wa habari

Ripoti zinaeleza kuwa, katika ajali zote mbili za Ethiopia na Indonesia zilizohusisha ndege ya Boeing 737 aina ya MAX8, ndege hizo zilibadilisha kimakosa kiwango cha masafa ya upaaji, ikiwa ni ishara kwamba marubani walikuwa wakihangaika kudhibiti hatamu za uongozaji wa ndege.

Aidha muda mfupi baada ya kuruka, marubani wa ndege ya Ethiopia na ile ya Lion Air waliripoti matatizo ya uongozaji ndege na kujaribu kurudi viwanja vya ndege lakini hatimaye ndege hizo zikaanguka.

Nchi kadhaa duniani zimeshasimamisha safari za ndege za Boeing 737 aina ya MAX 8 kufuatia ajali ya ndege hiyo inayomilikiwa na shirika la ndege la Ethiopia iliyotokea Jumapili ya tarehe 10 mwezi huu na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwemo ndani yake.

Kampuni ya ndege hizo inakabiliwa na changamoto ya kuthibitisha kama aina ya ndege zake hizo zina usalama wa kufanya safari za anga kutokana na shaka kuwa, kasoro za mitambo yake zimechangia ajali hizo mbili zilizotokea ndani ya muda wa chini ya miezi sita na kuteketeza roho za jumla ya watu 346.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu