Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Kimbunga cha Idai chaua zaidi ya watu 100 Zimbabwe na Msumbiji

March 18, 2019

Watu zaidi ya 100 wameaga dunia na wengine wengi hawajulikani waliko katika nchi za Msumbiji na Zimbabwe baada ya kimbunga cha tropiki cha Idai kuzikumba nchi hizo za kusini mwa Afrika na kusababisha mafuriko ya gharika na pepo kali.

 

Mamlaka za Zimbabwe zimesema, idadi ya waliofariki dunia kutokana na tufani huko mashariki mwa nchi imeongezeka na kufika watu 65 huku nchini Msumbiji ikiripotiwa kuwa watu 48 wamefariki katika maeneo ya kati ya nchi hiyo yaliyoathiriwa na janga hilo la kimaumbile.

 

Joshua Sacco, mbunge wa bunge la Zimbabwe kutoka wilaya ya Chimanimani, ambalo ni eneo lililoathiriwa vibaya zaidi na tufani ya Idai amesema, mbali na waliofariki, watu wengine kadhaa wanaokadiriwa kuwa ni kati ya 150 hadi 200 hawajulikani waliko baada ya nyumba na madaraja kusombwa na mafuriko ya gharika yaliyosababishwa na tufani hiyo.

 

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na kimbunga hicho yameshindikana kufikiwa hadi sasa, huku pepo kali  na mawingu mazito yakikwamisha safari za helikopta za uokozi za jeshi la Zimbabwe.

Wananchi wenye simanzi wakitazama nyumba zao zilizosombwa na mafuriko ya kimbunga cha Idai

 

Rais Emmerson Mnangagwa, ambaye amefupisha safari yake ya Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ametangaza hali ya maafa katika maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga.

 

Wakati huohuo watu 48 wameripotiwa kufariki dunia katika nchi jirani na Zimbabwe ya Msumbiji, ambayo ilikumbwa na tufani ya Idai kwa mara ya kwanza siku ya Alhamisi.

 

Ripoti zinasema, watu hao wamefariki katika mkoa wa Sofala, ambao ndio ulioathiriwa zaidi na tufani hiyo.

 

Siku ya Ijumaa, kimbunga cha Idai kiliyakumba pia maeneo ya kati ya Msumbiji na kukata mawasiliano kwa wakazi zaidi ya laki tano wa mji wa bandari wa Beira.

 

Kimbunga hicho kilisababisha kufungwa kwa muda pia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beira baada ya kuharibu mnara wa kuongoza safari za anga.

 

www.mzunguko.com

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload