Watu wasiopungua 49 wauawa katika mashambulio ya kigaidi dhidi ya misikiti miwili nchini New Zealand


Watu wasiopungua 49 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameuawa na wengine wasiopungua 48 wamejeruhiwa katika mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya misikiti miwili katika mji wa Christchurch nchini New Zealand wakati waumini wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya Sala ya Ijumaa hii leo.

Magaidi waliobeba bunduki za otomatiki wameshambulia misikiti miwili ya Al Noor na Linwood uliopo kwenye kiunga hicho cha mji wa Christchurch.

Vyombo vya habari vimewanukuu mashuhuda wakieleza kuwa mtu mmoja aliyevalia nguo nyeusi na helmeti, akiwa amebeba bunduki ya rashasha aliingia kupitia nyuma ya msikiti wa Al Noor na kuanza kuwafyatulia risasi kwa dakika kadhaa Waislamu waliokuwa kwenye Sala.

Majeruhi mmoja akikimbiziwa hospitali

Polisi imethibitisha kuuawa watu wasiopungua kumi katika msikiti wa Linwood wakati wa Sala ya Ijumaa ya leo.

Vyombo vya usalama vimewataka watu wabakie majumbani mwao sambamba na kuwatahadharisha Waislamu wasiende msikitini kwa sasa katika "sehemu yoyote ya New Zealand".

Vyombo vya habari vimeeleza kuwa hali ya hofu imetanda, huku damu za watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo la kinyama la kigaidi zikiwa zimetapakaa kila mahali katika maeneo ya misikiti hiyo.

Hali ya taharuki katika eneo la tukio

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern ameueleza mkutano wa waandishi wa habari kuwa, hujuma hizo zinaonekana kuwa ni "shambulio la kigaidi" lililopangwa kwa umakini.

Amesema tukio hilo la leo ni moja na litaendelea kuwa moja ya siku mbaya zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Wakati huohuo Polisi ya New Zealand imetangaza kuwa washukiwa wanne wa mashambulio hayo ya kigaidi, akiwemo mwanamke mmoja wametiwa nguvuni.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu