Mlipuko wa bomu waua watu wanane katika soko la mnada wa mifugo Somalia


Takribani watu wanane wameuawa nchini Somalia na wengine kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko wa bomu katika soko la kuuza na kununua mifugo kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Maafisa usalama nchini Somalia wanasema kuwa, wahanga wote wa shambulio hilo la bomu ni raia waliokwenda katika gulio hilo lililoko katika mji wa Bay kwa ajili ya kuuza na kununua mifugo.

Ripoti zaidi zinasema kuwa, watu wengine 40 wamejeruhiwa katika mlipuko huo wa bomu uliolenga soko hilo katika kijiji cha Goofgaduud.

Wakati huo huo, wanachama sita wa kundi la kigaidi la al-Shabab wameangamizwa baada ya ngome zao kushambuliwa na vikosi vya serikali ya Mogadishu.

Taarifa iliyotolewa na vikosi vya usalama vya Somalia imeeleza kuwa, wanamgambo sita wa kundi la kigaidi la al-Shabab wameuawa baada ya ngome zao kushambuliwa kusini mwa nchi hiyo. Aidha miongoni mwa waliouawa wamo makamanda watatu wa kundi hilo la kigaidi.

Kundi la kigaidi la al Shabaab mara kwa mara hufanya mashambulizi ya kulipua mabomu huko Mogadishu na katika maeneo mengine ya Somalia dhidi ya serikali na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMISOM.

Askari wa AMISOM walipelekwa Somalia mwaka 2007 kuangamiza kundi la kigaidi la al Shabab na kuilinda serikali ya nchi hiyo.

Wanajeshi karibu 21,000 wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu