Tanzania yasema imeimarisha usimamizi wa matumizi salama ya nyuklia


Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imefanikiwa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia nchini humo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekenolojia William Ole Nasha wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Waratibu wa Miradi ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia kutoka nchi 46 wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unaofanyika mjini Arusha.

Amesema shirika hilo linafadhili miradi mingi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, ambapo imewezesha kupatikana kwa vifaa muhimu vya utafiti wa tiba na maradhi ya saratani ambavyo vimefungwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa Bugando jijini Mwanza na Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Akihutubu katika mkutano huo wa siku tano utakaomalizika Machi 15, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi ya IAEA barani Afrika, Profesa Shaukat Abdulrazak amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia ya nyukilia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, kilimo, mifugo, maji, viwanda na ujenzi.

Mwishoni mwa mwaka jana, Kenya iliomba msaada wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuisaidia kuimarisha matibabu ya saratani katika hospitali mbili kubwa nchini humo na pia kueneza huduma hizo za matibabu katika miji mingine mitatu.

Waziri wa Nishati wa Kenya alihutubia kikao cha mawaziri cha IAEA mjini Vienna Austria na kufichua kuwa, nchi hiyo ya Afrika Mashariki iko mbioni kuunda kiwanda cha kuzalisha nishati ya nyuklia kwa ajili ya kuimarisha huduma za matibabu.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu