UN yatafakari kupunguza askari wake wa kulinda amani DRC


Huenda idadi ya askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO ikapunguzwa.

Hayo yamedokezwa jana Alhamisi na afisa wa ngazi za juu wa UN ambaye hakutaka kutaja jina lake ambaye anasisitiza kuwa, kupunguza idadi ya wanajeshi hao itakuwa ni hatua ya kwanza ya mchakato wa kukiondoa kikamilifu kikosi hicho cha kulinda amani nchini DRC.

Kwa mujibu wa afisa huyo, UN inatathmini suala la kukiondoa kikamilifu nchini Kongo DR kikosi hicho chenye wanajeshi 16,000, baada ya kufanyika uchaguzi uliohitimisha uongozi wa Rais Joseph Kabila mwezi Disemba mwaka jana.

Rais Kabila amekuwa akitoa mwito wa kuondolewa nchini humo askari hao wa kulinda amani wa UN, lakini mrithi wake Felix Tshisekedi amekuwa akisisitiza kuwa, kikosi hicho kinapaswa 'kuzatitiwa kwa silaha vilivyo.

Baraza la Usalama la UN linatazamiwa kurefusha muda wa kuhudumu kikosi hicho, ambacho hutengewa bajeti ya dola bilioni moja kila mwaka.

Askari wa MONUSCO wakishika doria Kongo DR

Machi mwaka jana baraza hilo lilikiongezea muda wa kuhudumu kikosi hicho hadi Machi mwaka huu 2019, ambapo mbali na majukumu yake ya kusimamia amani kilipaswa pia kusaidia mchakato na maandalizi ya uchaguzi mkuu ambao ulifanyika hivi karibuni.

Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO kimekuwa nchini humo tangu mwaka 1999.

Raia na mashirika mbalimbali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakikosoa utendaji wa kikosi hicho,mbali na askari wanaounda kikosi hicho cha MONUSCO mara kadhaa kukumbwa na kashfa za ngono na vitendo vya ubakaji.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu