The Guardian: Kuna viashiria vya hitilafu baina ya Mfalme Salman wa Saudia na mrithi wake


Gazeti la The Guardian la Uingereza limefichua kwamba, kuna viashiria vya hitilafu zinazoongezeka kila siku baina ya Mfalme Salman wa Saudi Arabia na mrithi wa kiti hicho ambaye ni mwanaye,

Muhammad bin Salman na kwamba hitilafu hizo zimeonekana waziwazi wakati wa safari iliyofanywa hivi karibuni na mfalme huyo wa Saudia huko Misri na maamuzi yaliyochukuliwa na mwanaye bila ya yeye kuwepo nchini.

Gazeti hilo la Uingereza limefichua kwamba, washauri wa Mfalme Salman wa Saudia walimtahadharisha wakati wa safari yake nchini Misri kwamba, kuna uwezekano wa kufanyika harakati dhidi ya uongozi wake na kwamba mfalme huyo alichukua hatua mara moja na kubadilisha maafisa wa usalama wa gadi inayomlinda.

Guardian limefuchua kuwa, mabadiliko hayo ya maafisa wa Gadi ya Mfalme wa Saudia yamefanyika kutokana na hofu kwamba, wale wa zamani wanamtii zaidi Muhammad bin Salman kuliko mfalme mwenyewe.

Gazeti hilo pia limefichua kwamba, wakati Mfalme Salman akiwa safarini nchini Misri kushiriki mkutano wa viongozi wa nchi za Kiarabu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari,

Muhammad bin Salman alichukua maamuzi mawili muhimu ya kumteua balozi mpya wa nchi hiyo huko Marekani na kumteua ndugu yake mwenyewe Khalid bin Salman kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi bila ya baba yake kuwa na taarifa.

Hatua hiyo imemkasirisha sana Mfalme Salman ambaye alipata habari hizo kupitia matangazo ya televisheni.

Mfalme Salman na mwanaye, Bin Salman

Hitilafu za sasa baina ya Mfalme wa Saudi Arabia na mwanaye, Muhammad bin Salman ambaye ndiye mrithi wa kiti cha ufalme zinaongezwa katika orodha ya hitilafu nyingine baina ya wawili hao ikiwa ni pamoja na jinsi Bin Salman anavyoshughulikia kadhia ya mateka wa vita huko Yemen,

msimamo wa serikali ya Riyadh kuhusu maandamano na ghasia zinazoendelea katika nchi za Sudan na Algeria dhidi ya viongozi wa nchi hizo na msimamo wa Saudia kuhusu kadhia ya Palestina.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu