Waziri wa Fedha wa Kenya asailiwa tena na Polisi kuhusiana na kashfa ya ujenzi wa mabwawa


Polisi ya Kenya imemwita kumsaili kwa mara ya pili Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Henry Rotich kuhusiana na kashfa ya mamilioni ya dola ya kutanguliza malipo kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa mabwawa mawili.

Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) George Kinoti, amethibitisha kuwa waziri Rotich amefika mbele ya maafisa wa idara hiyo mapema asubuhi ya leo na anatazamiwa kuandikisha maelezo.

Katika taarifa aliyotoa jana usiku kwa vyombo vya habari, Kinoti alisema waziri huyo anapaswa kutoa majibu kwa masuali kadhaa.

Wiki iliyopita, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Kenya ilitangaza kuwa inachunguza udanganyifu uliofanywa katika mradi wa ujenzi wa mabwawa mawili ya Kimwarer na Arror unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 63.

Baadhi ya malipo ya mradi huo tayari yameshatolewa wakati ujenzi wa mabwawa hayo bado haujaanza tangu mwaka 2017.

Mandhari ya Bonde la Ufa la Kerio

Katika taarifa iliyochapishwa na vyombo vya habari siku ya Jumapili, waziri huyo wa fedha wa Kenya alithibitisha kuwa shilingi bilioni 19.8, sawa na dola 198 za Marekani zimetangulia kulipwa kwa ajili ya mabwawa hayo yanayotazamiwa kujengwa katika kaunti ya Elgeyo Marakwet. Hata hivyo Rotich amesisitiza kuwa malipo hayo yametolewa kwa kufuata taratibu za sheria.

Mbali na waziri wa fedha, wengine wanaochunguzwa kuhusiana na kashfa ya ujenzi wa mabwawa hayo ni Mkurgenzi wa Uendeshaji wa Mamlaka ya Ustawi wa Bonde la Ufa la Kerio (KVDA) Kavid Kimisop na wajumbe wengine kadhaa wa bodi za Mashirika ya Umma, ambao tayari wameshasailiwa mara nne na Idara ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu