Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Wanafunzi Algeria wagoma kuingia madarasani kupinga msimamo mpya wa Bouteflika

March 5, 2019

Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Algeria ambao wameonyesha kuwa na dhamira ya kuongoza maandamano makubwa zaidi dhidi ya serikali kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa miaka kadhaa sasa,

 

jana waligoma kuingia madarasani ili kuonyesha upinzani wao kwa pendekezo la Rais Abdelaziz Bouteflika la kugombea tena urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao, lakini kutobaki madarakani kwa muhula wote endapo atachaguliwa tena.

Wanafunzi wa chuo kikuu kikubwa zaidi nchini Algeria cha Bab Ezzouar kilichoko mjini Algiers pamoja na vyuo vikuu vyengine kadhaa katika mji mkuu huo wa Algeria jana waligoma kuingia madarasani.

 

Wakati huo huo mamia ya watu wamefanya maandamano katika miji mbali mbali ya Algeria, nje ya mji mkuu Algiers, ambayo yanaendelea kwa takribani wiki ya pili sasa kupinga Bouteflika kuwania tena urais kwa kipindi cha tano.

Maandamano dhidi ya Bouteflika

 

Siku ya Jumapili, kiongozi huyo alitoa pendekezo, ambalo inaonekana kuwa lililenga kupoza moto wa upinzani dhidi ya azma yake ya kuendelea kubakia madarakani, alipotangaza kuwa endapo atachaguliwa tena ataitisha uchaguzi wa mapema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

 

Mashinikizo dhidi ya Rais Abdelaziz Bouteflika yamekuwa yakiongezeka, ambapo katika hatua ya karibuni Sidi Ferroukhi, waziri wa zamani wa kilimo na mbunge wa chama tawala cha FNL jana alitangaza kujiuzulu ubunge, ikiwa ni hatua ya nadra kushuhudiwa miongoni mwa wanachama waandamizi wa chama hicho.

Rais Abdelaziz Bouteflika, anayetembea kwa msaada wa kiti cha magurudumu

 

Sambamba na hatua hiyo, kundi moja la viongozi wa upinzani na wanaharakati wa kisiasa wametoa mwito wa kuakhirishwa uchaguzi ambao umepangwa kufanyika tarehe 18 ya mwezi ujao wa Aprili.

 

Wapinzani wa kiongozi huyo wanasema, Bouteflika hana uwezo tena wa kuendelea kuongoza nchi kutokana na afya yake kudhoofika na kwa sababu ya kile wanachokiita ufisadi sugu na kukosekana mageuzi ya kiuchumi ya kukabiliana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kinachopindukia asilimia 25 kwa vijana wenye umri chini ya miaka 30 nchini Algeria.

 

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82, anayetembea kwa kutumia kiti cha magurudumu amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload