Al-Shabaab yateka mji wa Somalia baada ya Kenya kuondoa wanajeshi wake


Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limeuteka mji mmoja wa kistratajia ulioko kusini magharibi mwa Somalia, baada ya jeshi la Kenya KDF kuwaondoa wanajeshi wake waliokuwa wanaudhibiti mji huo

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, genge hilo la kigaidi liliuteka mji wa Fahfahdhun, umbali wa kilomita 80 magharibi mwa mji wa Bardhere katika jimbo la Gedo, jana Jumamosi, muda mfupi baada ya askari wanaohudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani wa Umoja wa Afrika walioko Somalia (Amisom) kuondoka katika mji huo.

Mji huo umekuwa chini ya udhibiti wa KDF tokea mwaka 2012.

Amisom haijatoa taarifa kuhusu utekaji huo wa kwanza kabisa mwaka huu wa genge la kigaidi la al-Shabaab.

Wanajeshi wa KDF nchini Somalia

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu 29 kuuawa katika shambulizi la kigaidi la genge hilo katika mtaa wenye shughuli nyingi wa Makka Al-Mukarama katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Askari wapatao 21,000 wa Amisom hawajaweza kurejesha uthabiti na usalama kamili nchini humo hasa katika mji mkuu Mogadishu.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu