Ansarullah: Watoto na wanawake wa Yemen wanauawa kwa silaha za Marekani


Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema wanawake na watoto wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu wanauawa kikatili kwa silaha zilizoundwa na Marekani na Wamagharibi katika hujuma zinazoongozwa na Saudi Arabia na waitifaki wake.

Abdul-Malik al-Houthi aliyasema hayo jana Jumatatu katika hotuba iliyorushwa mubashara kwa njia ya televisheni kutoka mji mkuu Sana'a na kubainisha kuwa, "Lengo la maadui wa Uislamu katika uvamizi wa hivi sasa dhidi ya Yemen ni kuidhibiti nchi hiyo kikamilifu."

Amesema Uislamu ulikuja kupambana na utumwa, lakini maadui wanaelekeza nguvu zao zote kumuhujumu mwanamke ambaye ana nafasi na jukumu muhimu katika familia na jamii.

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen anasisitiza kuwa, "Uislamu ulikuja kutupa uhuru na kutuondoa katika minyororo ya utumwa na utegemezi."

Sehemu ya athari za uvamizi wa Saudia dhidi ya Yemen

Abdul-Malik al-Houthi alitoa hotuba hiyo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Fatima (AS), binti ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo huadhimishwa kama Siku ya Wanawake katika nchi za Kiislamu.

Amesema, "Wale wanaojiita watetezi wa haki za wanawake ndiyo tishio kuu kwa wanawake kutokana na sera zao. Wanawake na watoto wanauawa kikatili kwa kutumia silaha za Marekani na Wamagharibi nchini Yemen."

Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa makumi ya maelfu ya watu waliopoteza maisha katika vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel, tokeo Machi mwaka 2015.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu