Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Uchaguzi Nigeria: Buhari aongoza, upinzani wapinga matokeo

February 26, 2019

Tume ya Uchaguzi Nigeria imetangaza kuwa Rais Muhammad Buhari anaongoza kwa kura 280,000 katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumamosi iliyopita.

 

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria (INEC) ametangaza kuwa, Rais Buhari mwenye umri wa miaka 76, wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC) anaongoza kwa asilimia 51 ya kura, akifuatia na mshindani wake wa karibu mgombea wa upinzani Atiku Abubakar (72)  wa chama cha People's Democratic Party (PDP), ambaye amezoa asilimia 45.8 ya kura kufikia sasa.

 

Kufikia jana usiku, matokeo ya majimbo 11 kati ya 37 ya nchi hiyo yalikuwa yamehesabiwa na shughuli hiyo inaendelea leo saa nne asubuhi kwa saa za nchi hiyo.

 

Hii ni katika hali ambayo, chama cha mgombea mkuu wa upinzani Atiku Abubakar ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Nigeria kimepinga matokeo hayo.

Mwenyekiti wa chama hicho Uche Secondus amesema matokeo yanayoendelea kutangazwa hayakubaliki,  na kwamba Tume ya Uchaguzi ikishirikiana na chama cha Rais Buhari, kimechakachua matokeo ya mwisho yanayowasilishwa katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha matokeo.

 

Msemaji wa  Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria Rotimi Oyekanmi hata hivyo anasisitiza kuwa mchakato wa uchaguzi umesimamiwa na waangalizi wa ndani na wa nje, na matokeo yanayotolewa ni halali na yanaakisi matakwa ya wapiga kura. 

 

Wanigeria wanaendelea kusubiri matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo katika hali ambayo, makundi ya asasi za kiraia za waangalizi wa uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumamosi yameripoti kuwa, machafuko yanayohusiana na uchaguzi yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 39.

 

www.mzunguko.com

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload