"Kuna ushahidi wa wazi wa kuwepo mashirikiano ya siri baina ya Russia na timu ya kampeni ya Tru


Adam Schiff, mwenyekiti wa kamati ya intelijensia ya Baraza la Wawakilishi la Marekani amesema, kuna ushahidi mkubwa na wa wazi unaothibitisha kuwa timu ya kampeni ya rais wa nchi hiyo Donald Trump ilikuwa na mashirikiano ya siri na Russia wakati wa uchaguzi wa rais wa mwaka 2016.

Matamshi hayo ya Adam Schiff, ambaye ni mbunge kwa tiketi ya chama cha Democrat yanagongana na maelezo ya Richard Burr, mwenyekiti wa kamati ya intelijensia katika Seneti ya nchi hiyo kutoka chama cha Republican ambaye amesema, hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa timu ya kampeni ya Trump ilikuwa na mashirikiano ya siri na Warussia.

Adam Schiff, mwenyekiti wa kamati ya intelijensia ya Baraza la Wawakilishi la US

Mnamo wiki iliyopita, Seneta Burr alitangaza kuwa, kamati anayoiongoza haijapata kitu chochote kinachoonyesha kuwa kulikuwako na mashirikiano ya siri kati ya Russia na Trump.

Hata hivyo Seneta Mark Warner wa chama cha Democrat, ambaye ni naibu mwenyekiti wa kamati hiyo ya intelijensia ya Seneti alipinga na kulalamikia matamshi hayo ya Burr.

Kadhia ya kuwepo mashirikiano ya siri kati ya timu ya kampeni ya Donald Trump na Russia wakati wa uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016 ingali ni moja ya masuala yenye mvutano mkubwa katika anga ya siasa za Marekani.

Serikali ya Moscow imekuwa ikisisitiza kila mara kuwa haijaingilia kwa namna yoyote ile uchaguzi wa rais wa Marekani.


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu