Erdogan aapa kufuatilia mauaji ya Khashoggi katika mahakama ya kimataifa


Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema nchi yake iko mbioni kupeleka kesi ya mauaji ya mwanahabari mpinzani wa utawala wa Saudia Jammal Khasoggi katika mahakama ya kimataifa.

Katika mahojiano yake na televisheni ya A-Haber, Erdogan amesema serikali yake ina azma ya kupeleka kesi ya mauaji ya Khashoggi katika mahakama ya kimataifa na ametaka Marekani itoe mchango wake katika kesi hiyo.

Erdoan ameikosoa vikali Marekani kwa kupuuza mauaji ya kinyama ya Khashoggi kwa sababu tu ya uhusiano wake wa karibu na utawala wa Saudi Arabia.

Jamal Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa familia ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, aliuliwa na maafisa wa utawala huo na mwili wake kukatwa vipande vipande baada ya kuingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe 2 Oktoba mwaka uliopita. Hadi hivi sasa Saudia imekataa kukabidhi angalau mabaki tu ya mwili wa mwandishi huyo.

Ushahidi na nyaraka zote zilizopo, zikiwemo taarifa zilizotolewa na serikali ya Uturuki na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) zinaonyesha kuwa Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ndiye mpangaji mkuu wa jinai hiyo ya kutisha.

Rais Erdogan wa Uturuki

Hivi karibuni Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema maafisa wa Saudi Arabia wanahusika moja kwa moja na mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa akiukosoa utawala huo wa kifalme.

Agnès Callamard, mchunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa aliyeongoza timu maalumu ya uchunguzi na upelelezi wa mauaji ya Khashoggi amesema katika ripoti yake aliyotoa Februari 7 kuwa, ushahidi unaonyesha kuwa mwandishi huyo wa habari ni mhanga wa mauaji ya kikatili ambayo yalipangwa na kutekelezwa na maafisa wa Saudi Arabia.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu