Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Kutiwa mbaroni wanaharakati wa kike Saudia, sehemu ya ukandamizaji wa Bin Salman

February 15, 2019

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Saudi Arabia imewakamata na kuwatia korokoroni makumi ya wanaharakati wa kike wa kutetea haki za wanawake na kuwatuhumu kuwa wameisaliti nchi, kudhuru maslahi ya taifa na kuwaunga mkono kifedha na kiroho maadui wa nchi hiyo.

 

Wanaharakati hao wamekuwa wakifanya jitihada za kutetea haki za kijamii na kiraia na kupinga dhulma na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya wanawake wenzao nchini Saudi Arabia.

 

Ripoti za mashirika na kutetea haki za binadamu zinaonesha kuwa, idadi ya wafungwa wa kike wa kisiasa imeongezeka sana nchini Saudi Arabia.

 

Wafungwa hawa wa kike ni sehemu ndogo ya maelfu ya wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika korokoro za utawala wa kifalme wa Saudia.

 

Hivi karibuni kamati ya Bunge la Uingereza ilifichua kuwa, wanaharakati wa kike wanaoshikiliwa katika korokoro za Saudia wanafanyiwa ukatili mkubwa na udhalilisha wa kutisha.

 

Vilevile gazeti la Marekani la Washington Post limeripoti kuwa, wafungwa wa kisiasa wa kike wa Saudia wanashikiliwa katika seli na vyumba vya mtu mmoja mmoja na kuteswa kinyama. 

 

Awali shirika la kutetea haki za binadamu la al Qist lilichapisha ripoti mpya kuhusu ukandamizaji na ukatili wanaofanyiwa wafungwa wa kisiasa wa kike katika korokoro za Saudia na kufichua kwamba, wafungwa hao wanapewa mateso ya kinyama na kwamba baadhi ya mateso hayo yanasimamiwa na watu wa karibu kwa Mrithi wa Ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman.

Wimbi la malalamiko kuhusu jinai na ukatili unaofanywa na utawala wa kifalme wa Saudia dhidi ya mahabusu wa kike limepanuka sana na kuingia hata katika nchi za Magharibi.

 

Wawakilishi wa vyama vya Democratic na Republican katika Kongresi ya Marekani sasa wamewasilisha muswada wa azimio linaloitaka serikali ya Saudi Arabia kuwaachia huru wanaharakati wa kike wanaoshikiliwa katika korokoro za nchi hiyo haraka iwezekanavyo na bila ya masharti yoyote. 

 

Hatua hiyo ya wabunge wa Marekani imechukuliwa kutokana na mashinikizo makubwa ya raia wa nchi hiyo wanaopinga ukandamizaji wa serikali ya Saudia. 

 

Chini ya uongozi wa Bin Salman, Saudi Arabia imevuka mistari yote myekundu ya haki za binadamu, na kinyume na propaganda zinazofanywa na mrihi huyo wa kiti cha ufalme,

 

walimwengu wanaendelea kushuhudia ukiukwaji mkubwa na wa kutisha wa haki za wanawake na raia wa Saudi Arabia na nchi jirani kwa ujumla.

Wanaharakati wsa kike Saudia wanateswa kinyama

 

Mwanamke nchini Saudia hana haki ya kufanya shughuli za kiuchumi, kiutalii na kwa ujumla haki za kimsingi kabisa za kijamii. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, mwaka 2016 Baraza la Masuala ya Kijamii na Kiuchumi la Umoja wa Mataifa liliichagua Saudia kuwa mwanachama katika kamati yake ya wanawake kwa kipindi cha miaka minne!

 

Hatua hiyo ilichukuliwa licha ya Saudi Arabia kushika nafasi ya 141 kati ya nchi 144 kwenye vigezo vya kimataifa vya hitilafu za kijinsia vya Baraza la Haki za Wanawake la Umoja wa Mataifa katika mwaka 2016.

Udiplomasia wa fedha za mafuta wa Saudia unafunga vinywa na taasisi za kimataifa za haki za binadamu.

 

Hatua ya Saudi Arabia ya kupewa uanachama katika Kamati ya Haki za Wanawake ya Umoja wa Mataifa imeonesha kwamba, jumuiya za kimataifa za haki za binadamu zimekuwa mateka wa udiplomasia wa fedha za mafuta za utawala huo wa kifalme na misimamo ya kindumakuwili ya madola ya Magharibi kuhusiana na suala la haki za binadamu.

 

www.mzunguko.com

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload