Watu kadhaa wapoteza maisha katika mkanyagano nchini Nigeria


Watu wasiopungua 14 wameaga dunia katika mkanyagano uliotokea katika mkutano wa kisiasa kusini mwa Nigeria.

Mashuhuda wanasema mkanyangano huo ulitokea jana Jumanne katika mkutano wa kampeni za uchaguzi za chama tawala cha Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo, katika mji wa bandari wa Harcourt, jimboni Niger Delta kusini mwa nchi.

Judith Amaechi, mkuu wa timu ya vijana na wanawake wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC) katika jimbo hilo ameeleza juu ya kusikitishwa kwao na tukio hilo, lililosababisha wanachama na wafuasi kadhaa wa chama hicho kupoteza maisha

Hata hivyo hajabainisha idadi ya watu walioaga dunia katika mkanyagano huo, lakini baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa ni watu 14.

Matukio ya aina hii yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara nchini humo, haswa katika kipindi hiki cha kampeni za lala salama.

Rais Muhammadu Buhari (kulia) na Atiku Abubakar watakaochuana katika uchaguzi wa rais.

Watu wengine kadhaa waliuawa wiki iliyopita katika mkanyagano mwingine wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais katika jimbo la Taraba lililoko mashariki mwa nchi.

Nigeria ambayo ni nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika na yenye utajiri wa mafuta inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa rais na bunge Jumamosi ijayo.


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu