Wanaotekeleza ukatili dhidi ya wanawake na walio na ulemavu wa ngozi wawajibishwe-OHCHR

January 26, 2019

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imeelezea kusikitishwa na ongezeko la vitendo vya ghasia za kisiasa, ukatili dhidi ya wanawake na mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Malawi, wakati huu uchaguzi ukitarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu wa 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari, mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa OHCHR, Rupert Colville ametaja baadhi ya matukio yaliyotekelezwa ikiwemo mbunge wa Malawi, Bon Kalindo ambaye alikamatwa kwa madai ya kumtukana rais ambapo baadaye aliachiwa huru lakini yaelezwa kuwa alivamiwa na wanaodaiwa kuwa vijana wanachama wa Democratic Progressive Party (DPP) kwenye makazi ya kamishna wa wilaya katika mji wa kusini wa Mulanje.

Bwana Colville amesema ukatili umeongezeka tangu uchaguzi wa awali wa 2018, ambapo wagombea wanawake walikabiliwa na vitisho na mateso ikiwemo wapiga kura wanawake.

Msemaji huyo amesema visa vya mashambulizi dhidi ya watu walio na ulemavu wa ngozi vimeongezeka kuelekea uchaguzi.

 

“Matukio ya hivi karibuni ni pamoja na mauaji ya Yasin Phiri, mwanamume wa miaka 55 aliyekuwa na ulemavu wa ngozi huko Kaskazini mwa Malawi Desemba 31 ambapo alidungwa kisu mbele ya mtoto wake kabla ya kutolewa nyumbani kwake na kukatwa mikono.

 

Na siku tatu zilizopita Januari 22, mtoto wa mwaka mmoja alitekwa nyara na hajulikani aliko”.

 

Kwa mantiki hiyo OHCHR inatoa wito kwa mamlaka kuimarisha juhudi zake kulinda watu walio na ulemavu wa ngozi na kuwashtaki na kuwawajibisha wanaodaiwa kutekeleza uhalifu huo.

 

www.mzunguko.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon