Manusura wa ebola DRC wasaidia kulea watoto yatima


Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mlipuko wa mwaka jana wa ebola kwenye majimbo ya Equateur na Kivu Kaskazini yameacha takribani watoto 400 yatima au kutengwa na familia zao na hivi sasa manusura wa ugonjwa huo wamechukua hatua ya kuwalea.

Katika kituo kimoja cha kutibu Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC anaonekana Kavira, mwanamke manusura wa ugonjwa wa Ebola akiwa anabembeleza mtoto Josue baada ya kumnywesha maziwa. Kavira aligua Ebola lakini alipona na anasema…

“Nilipona kwasababu nilitunzwa vizuri. Baada ya kupona waliniuliza, kama wanavyouliza manusura wote wa ebola, kama umepona basi nije hapa kulea watoto ambao mama zao ni wagonjwa''

Kituo hiki kilichofunguliwa mwezi Novemba mwaka jana kina majengo yenye michoro ya kuvutia kwa watoto na hadi sasa kimeshalea zaidi ya watoto wachanga 20.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake wanashirikiana na manusura wa Ebola kulea watoto ambao wazazi wao bado wanapatiwa matibabu dhidi ya ebola.

“Nauelewa huu ugonjwa na nafahamu kile ambacho mama yake anapitia. Iwapo sitamtunza vyema huyu mtoto, mtoto hatokuwa na furaha. Napaswa kumlea vyema kama ambavyo mama yake angalifanya. Na mimi nafurahi sana nikicheza naye, tunalala, namlisha chakula, nafurahi sana.”

Jambo la kusikitisha ni kwamba mama mzazi wa Josue alifariki dunia kwa ebola na baba yake angali anapata matibabu.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu