Mafuriko katika makazi ya wakimbizi Lebanon ni tabu juu ya tabu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi UNHCR linatoa msaada wa dharura kwa wakimbizi wa Syria walioko nchini Lebanon baada ya mvua kubwa kunyesha katika nchi hiyo.

Wakimbizi wanaonekana katika video wakiwa wamebeba magodoro na mahema, Hiba Fares, afisa habari wa UNHCR anaeleza.

Katika bonde la Bekaa nchi Lebanon kwenye makazi ya wakimbizi kutoka Syria, wanaonekana watoto wakijaribu kuvuka katika mitaa ya mahema yaliyozungukwa na maji kila upande nje na ndani.

Watoto wakitembea wanajishikiza katika mahema yaliyochanika na wengine wameamua kutembea tu katika maji kwani hakuna paliposalia, na juhudi za kujaribu kukwepa maji zimeshagonga mwamba.

Hiba Fares, afisa habari wa UNHCR anasema shirika limekuwa likijaribu kuzisaidia familia zilizoathiriwa na mafuriko. Ameongeza kuwa mahema ya baadhi ya watu yamechanika au kukatika na wengine wamelazimika kuhamia katika mahema ya majirani au ndugu zao.

UNHCR inakadiria kuwa wakimbizi 50,000 wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi yapatayo 850 wanaweza kuathirika na mafuriko. Hakuna majeruhi ambao wameripotiwa hadi kufikia sasa.

Nchini Lebanon, maisha ni mahangaiko ya kila siku kwa zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Syria ambao wana vyanzo kidogo au hawana kabisa vyanzo vya mapato.

Hakuna kambi rasmi za wakimbizi na matokeo yake wakimbizi hao wametapakaa katika maeneo mbalimbali mara nyingi wakitumia malazi na familia nyingine za wakimbizi katika maeneo yaliyojaa watu wengi sana.

Tangu mwaka 2011, Zaidi ya watu milioni 5.6 wameikimbia Syria na kuingia katika nchi jirani au mbali Zaidi. Wengine wameishia katika katika mipaka ya nchi yao. Mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake wameomba dola bilioni 5.5 za kimarekani ili kuweza kutoa misaada ya kibinadamu duniani kote mwaka huu.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu