Matokeo ya uchaguzi DRC yakisubiriwa, hali ni tulivu ila tete- OHCHR


Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesema hali nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ni tulivu ila tete wakati huu ambapo matokeo ya uchaguzi mkuu yanasubiriwa na wananchi wa nchi iyo.

Huku kukiwa na ripoti ya kwamba waandishi wa habari na wagombea kutoka vyama vya upinzani wanakumbwa na vitisho na kuna vizuizi kuelekea katika baadhi ya vyombo vya habari, ofisi hiyo kupitia msemaji wake, Ravina Shamdasani imeonya kuwa hatua zozote za kuziba mdomo wapinzani zitakuwa na madhara

Kauli ya Bi. Shamdasani imekuja saa chache kabla ya mashauriano ya faragha kuhusiana na uchaguzi huo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

Matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 30 mwezi uliopita wa Desemba ukihusisha wagombea 21, yanatarajiwa kutangazwa jumapili hii ingawa tume ya uchaguzi DRC imesema kuwa inawezekana tarehe ikasogezwa mbele.

“Kile ambacho wenzangu wamenijulisha ni kwamba ingawa hali ni tulivu bado ni tete kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi,” amesema msemaji huyo wa OHCHR akiongeza kuwa taarifa za awali zinaripoti matukio ya hapa na pale ya ghasia na baadhi ya watu wamejeruhiwa.

OHCHR imekuwa na ofisi yake kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu Afrika lakini haijawa na dhima yoyote katika usimamizi wa uchaguzi huo ambao ulikuwa unaahirishwa tangu mwaka 2016

Upigaji kura hata hivyo uliahirishwa hadi mwezi Machi mwaka huu katika wilaya tano kutokana na ukosefu wa usalama na mlipuko wa Ebola.

Sambamba na hayo, Bi. Shamdasani ameripoti uwepo wa ukiukwaji wa haki za raia ikiwemo kukatwa kwa huduma za intaneti akitolea mfano matangazo ya radio ya RFI ya Ufaransa pamoja na Televisheni ya Canal Congo inayomilikiwa na kiongozi wa upinzania Jean-Pierre Bemba nayo ilikumbwa na mushkeli.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu