Airbus A220-300: Ndege mpya itakayonunuliwa na Tanzania ni ndege ya aina gani?


Ndege mpya ambayo itakuwa karibuni zaidi kununuliwa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kutumiwa na Shirika la Ndege la Air Tanzania inakaribia kukamilika kutengenezwa.

Ndege hiyo, ambayo inaundwa na kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus, itakuwa ya muundo wa A220-300

Ndege hiyo itakuwa na jina la Dodoma, mji mkuu rasmi wa Tanzania. Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa kuhamishia shughuli zake zote jijini Dodoma

Tanzania iliponunua ndege ya majuzi zaidi, 787-8 Dreamliner ya kampuni ya Boeing, ndege hiyo ilipewa jina la Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika.

Sawa na ndege hiyo ya Dreamliner, ndege hiyo mpya ya Airbus ina nembo ya 'Hapa Kazi Tu' chini ya jina Dodoma.

Hapa Kazi Tu imekuwa kauli mbiu ya Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli tangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015.

Kampuni ya Airbus Alhamisi iliandika ujumbe kwenye Twitter: "Kiwango cha joto ni chini ya sifuri hapa Mirabel, Canada lakini twiga kutoka Kilimanjaro huwa hawaingiwi na wasiwasi kutokana na baridi! Tunazindua rangi mpya za #A220 za @AirTanzania, ambao karibuni watakuwa shirika la kwanza la Afrika kuwa na ndege aina ya A220

Mirabel ni kisiwa kinachopatikana eneo la Montreal, kusini mwa Quebec ambapo zinapatikana karakana za Airbus.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu