Mjukuu wa Mangi Meli afanyiwa vipimo vya kinasaba DNA ili kutafuta fuvu la babu yake na Mtemi wa Wac


Mjukuu wa Mangi Meli, amefanyiwa vipimo vya kinasaba vitakavyosaidia kusaka fuvu la chifu huyo aliyenyongwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1900

Mangi Meli alinyongwa baada ya kuongoza mapambano dhidi ya utawala wa kikoloni na baadae kichwa chake kukatwa na kupelekwa Ujerumani.

Fuvu lake yawezekana kuwa ni moja kati ya mafuvu mengi yaliyopo kwenye makumbusho moja kubwa jijini Berlin.

Wanaharakati wanataka fuvu hilo lirejeshwe ili lipate mazishi ya heshima anayostahili kama shujaa nyumbani kwao Moshi, kaskazini ya Tanzania.

Isaria Meli, mwenye miaka 87 ni mjukuu wa Chifu huyo wa jamii ya Wachaga amezitaka serikali za Tanzania na Ujerumani kushirikiana ili kuwezesha kupatikana na kurejeshwa kwa fuvu hilo.

isaria alifanyiwa vipimo vya DNA jijini Berlin baada ya kukaribishwa na Wakfu wa Urithi wa Utamaduni wa Prussia (maarufu kama SPK) ambao unahifadhi mabaki ya mafuvu yalichukuliwa na wakoloni wa Kijerumani.

SPK tayari imeorodhesha mafuvu sita ambayo yanaaminika kutokea Moshi na yalihifadhiwa katika kipindi ambacho Chifu huyo aliuawa.

Mafuvu yote hayo yameandikwa "Dschagga/Wadschagga" ikimaanisha Wachaga, ambalo ndilo kabila la Mangi Meli.

Watafiti wataangalia kama vinasaba vya DNA vya Isaria vitaendana na moja ya mafuvu hayo. Majibu yanatarajiwa kupatikana ndani ya miezi sita ya mwanzo ya mwaka ujao, 2019.

Ujerumani na mafuvu kutoka Afrika

Mwanzoni mwa karne iliyopita, maelfu ya mafuvu kutoka makoloni ya Mjerumani ya Afrika yalipelekwa Berlin. Mafuvu hayo yalikuwa ni sehemu ya utafiti wa kibaguzi ambao hivi sasa unalaaniwa.

Baada ya kupitia katika mikono tofauti ya umiliki, mafuvu hayo 5,500 ikiwemo 200 kutoka Tanzania yalikabidhiwa kwa SPK mwaka 2011.

Wakfu huo sasa unachunguza sehemu hasa mafuvu hayo yalipotokea.

Mpaka sasa bado ni kitendawili kujua hasa ni nini kilitokea kwa fuvu la Mangi Meli ambalo limepotea.

www.mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu