MAKONDA ASEMA HAJUI CHOCHOTE KUHUSU MAKONTENA 20 YANAYOSHIKILIWA BANDARINIMkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amesema hajui chochote kile kuhusu kudaiwa au makontena yaliyokamatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato (TRA), imetangaza kusudio la kupiga mnada kontena 20 za Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa atashindwa kuzilipia ushuru na kuzichukua ndani ya siku 30 kuanzia Jumatatu. Kontena hizo za Makonda ambazo zimesubiri utaratibu wa kuzitoa TRA kwa zaidi ya siku 90 zinazokubalika kwa mujibu wa sheria za kodi, zimesheheni samani za ndani na ofisini. Awali, TRA ilitoa tangazo katika gazeti la Daily News, ikisema mtu aitwaye Paul Makonda bila kubainisha kama mtajwa ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam au la, anamiliki makontena 20 yenye bidhaa mbalimbali zikiwamo samani katika bandari kavu ya DICD. Hata hivyo, akizungumza jana wakati akizindua kamati ya mapendekezo kuhusu wanawake waliotelekezwa na wenza wao, Makonda alisema hajui chochote na amesikia habari hizo kwenye magazeti kama walivyozisikia watu wengine. “Sidhani kama nahusika na jambo lolote lile na sijui chochote, hilo unalolisema hata mimi nimesoma kwenye magazeti kama ulivyosoma wewe. Nafikiri zilikuwa ni habari za jana na leo nimesoma nyingine,” alisema. Makonda alisema Serikali hufanya kazi zake kwa maandishi na yeye hana nakala yoyote inayohusiana na mzigo huo. “Sio suala la kwangu kabisa, nimekusikia wewe kama mimi nilivyosikia jana (juzi) na ninafikiri tutaendelea kusikia hivyo hivyo na ndio maana katika hizo habari hakuna sehemu yoyote umeona nimenukuliwa kusema kama ni mali zangu,” alisema Makonda.

Ilielezwa kuwa samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh2 bilioni, zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council. Mei, 12 kaimu kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye alisema wamiliki wa mizigo hiyo wanatakiwa kuikomboa ndani ya siku 30 kuanzia siku hiyo. Katika tangazo hilo lenye orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda limejitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yakiwa na bidhaa kadhaa, zikiwamo samani. Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo aliliambia Mwananchi juzi kuwa mamlaka hiyo imetoa notisi ya siku 30 kwa waagizaji wa mizigo ambayo imekaa bandarini kwa zaidi ya siku 90. “Tangazo lililotolewa ni notice (taarifa) kwa wahusika ili wakomboe mizigo yao ndani ya siku 30. Isipokombolewa itanadiwa. Mizigo hiyo inaweza kuwa ni ile ambayo haijalipiwa kodi au hata ile iliyolipiwa lakini haijaondolewa,” alisema. Alipoulizwa kama shehena hiyo ni mali binafsi ya Makonda au ya ofisi yake, Kayombo alisema: “Majina yaliyoandikwa kwenye magazeti ndiyo taarifa za consignees (wapokeaji) zilizopo kwenye nyaraka.”CHANZO.Mwanachi Mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu