MAAMUZI YA KAMATI YA BODI YA LIGI HAYA HAPA

April 26, 2018

 

 

 

 

MAAMUZI YA KAMATI YA SAA 72

Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ya Bodi ya Ligi katika kikao chake kilichopita ilipitia taarifa na matukio mbalimbali na kufanya uamuzi ufuatao;

Mechi namba 171 (Njombe Mji 0 vs Simba 2). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonyesha vitendo vinavyoashiria ushirikina katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 3, 2018 kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, ikiwemo pia mshabiki mmoja wa timuhiyo kuingia uwanjani na kuchukua taulo la kipa wa Njombe Mji lililokuwa golini. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.

 

Mechi namba 165 (Mtibwa Sugar 0 vs Simba 1). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho ya mechi hiyo iliyofanyika Aprili 9, 2018 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

 

Kitendo hicho cha washabiki wa Simba iliyokuwa ikicheza ugenini ni ukiukaji wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, wakati adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi namba 177 (Singida United 0 vs Mtibwa Sugar 3). Mchezaji Tafadzwa Kutinyu wa Singida United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kufanya vitendo vyenye kuonyesha imani za ushirikina katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 6, 2018 kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

 

Katika mchezo huo, Kutinyu alichukua taulo la kipa wa Mtibwa Sugar na kulirusha jukwaani kwa washabiki wa Singida United ambao waliondoka nalo. Adhabu dhidi yake imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.

 

Mechi namba 184 (Mbao 0 vs Lipuli 0).Klabu ya Mbao imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mshabiki wake kuingia uwanjani na kuchukua glovu za akiba za kipa wa Lipuli zilizowekwa golini na kukimbia nazo, kitendo kinachoonyesha imani za kishirikina.

 

Adhabu dhidi ya Mbao katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 6, 2018 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.

mzunguko.com

 

 

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon