WAZIRI WA HABARI Dkt. HARRISON MWAKYEMBE ASHIRIKI KWENYE UFUNGUZI WA MASHINDANO YA SHIRIKISHO LA MIC


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe leo tarehe 22 Novemba, 2017 amekuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika, Taasisi na Makampuni ya Umma na Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) yanayofanyika kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa Samora mkoani Iringa.

Akifungua mashindano hayo Waziri Mwakyembe ameyashukuru mashirika na taasisi zilizoshiriki mashindano hayo kwa kuunga mkono dhamira ya Serikali ya Awamu ya 5 katika kukuza michezo nchini.

Aidha, Waziri Mwakyembe alielezea kutoridhishwa na tabia ya baadhi ya mashirika na taasisi kutoshiriki kwenye mashindano haya kwa kusingia sababu mbalimbali.

"Nitamjulisha Mlezi wa Kitaifa wa SHIMMUTA, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu changamoto zinazotokana na mashirika/taasisi za Serikali ambazo zimekuwa zikikacha kushiriki kwenye mashindano hayo pamoja na kutambuliwa rasmi kwa mashirika/taasisi zinazoshiriki", alisisitiza Waziri Mwakyembe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMMUTA Bw. Hamis Mkanachi alimuomba Waziri Mwakyembe kulisidia Shirikisho hilo kwa kufanikisha ushiriki wa mashirika na taasisi za Serikali ambayo yamekuwa hayashiriki kwa muda, pamoja na kuwaunganisha SHIMMUTA na Shirikisho lililopo upande wa Zanzibar.

Hapo awali akitoa salamu za mkoa, Mkuu wa Mkoa Mhe. Amina Masenza aliwakikishia washiriki usalama, amani na ulinzi katika kipindi chote cha mashindano pamoja huduma bora za kijamii.

Aidha, Mhe. Masenza aliwakumbusha washiriki kwenda kujionea vivutio vya kitalii na kihistoria vilivyopo mkoani Iringa yakiwemo maeneo ya Isimila, Kalenga na hifadhi ya Ruaha.


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu