Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

FAHAMU TATIZO LA PUMU

November 3, 2017

 

 

 

Pumu ni ugonjwa ambao huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu.  Ni ugonjwa ambao hushambulia watu wa jinsia zote na rika zote lakini mara nyingi zaidi watu hupata ugonjwa huu utotoni.

 Watoto wengi huanza kupata dalili za ugonjwa huu wanapofikia umri wa miaka mitano. Watoto walio kwenye hatari kubwa zaidi ya kupatwa na maradhi haya ni wale wanaozaliwa wakiwa na uzito mdogo, wale wanaolelewa kwenye mazingira yenye moshi wa sigara na wale wanaozalia kwenye familia zenye kipato kidogo.

 Mambo mengine yanayochangia ni mtoto kuwa na mzio (allergy) wa kitu fulani na/au kuzaliwa na wazazi wenye asili ya kuwa na maradhi haya. Watoto wa kiume hupata ugonjwa huu zaidi ya watoto wa kike lakini hali hubadilika wanapokuwa wakubwa. Katika ukurasa huu tutaona ni nini tiba ya pumu na jinsi ya kufanya ukiwa na ugonjwa huu ili uweze kuishi na kufanya shughuli zako za maisha bila kusumbuliwa na maradhi haya.

.Vyanzo ama vihatarishi vya pumu vimeeleweka kuwa ni kama ifuatavyo:

1. Mzio (Allergy):

 Karibu watu wote wenye pumu wana mzio (allergy) ambayo ni hali ya miili yao kutopenda vitu fulani pale vinapovutwa na hewa mtu anapopumua, vikiliwa, vikiingizwa mwilini kwa kudungwa sindano au vikigusa ngozi zao.

 Lolote likitokea katika hayo mtu mwenye mzio anaweza akawashwa macho, akatokwa na kamasi, akapumua akitoa sauti ya vifilimbi, akatokwa na vjipele juu ya ngozi au akapata tumbo la kuharisha.

 Baadhi ya vitu vinavyosababisha hali hiyo (allergens) ni protini za wanyama, poleni ya mimea, nyasi, vumbi, mende na baadhi ya madawa.

2. Uchafuzi Wa Mazingira:

 Dalili nyingi za pumu zinatokana na uchafuzi wa mazingira na hasa wa majumbani kutokana na mvuke unaotokana na vifaa vya kusafishia nyumba na rangi za kutani.

 Majiko ya kupikia yanayotumia gesi yanayotoa hewa aina ya nitrogen oxide ambayo pia huhusishwa na tatizo la pumu. Watu wanaopika kwa kutumia gesi hupatwa na matatizo yanayoambatana na pumu kama kupumua kwa shida na kubanwa na pumu.

Vitu vingine kwenye mazingira vinavyoaminika kusababisha pumu ni sulfur dioxide, nitrogen oxide, hali ya hewa ya baridi na hali ya kuwa na unyevunyevu mwingi katika hewa (high humidity).

3. Uzito Kupita Kiasi:

 Watu wazima wenye uzito mkubwa sana wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata pumu ukilinganisha na wale wenye uzito wa kawaida. Utafiti unaonyesha kuwa hatari ya kupata pumu isiyotokana na mzio (nonallergic asthma ) ni kubwa zaidi kuliko ile inayotokana na mzio (allergic asthma).

4.Ujauzito Na Uzazi:

 Jinsi uliovyoingia katika dunia hii ina uhusiano na uwezekano wa kupata pumu baadaye. Watoto waliozaliwa kwa operesheni wana asilimia 20 zaidi ya uwezekano wa kupata pumu baadaye – inawezekana kuwa maambukizi yanayoathiri kinga za mwili kutokana na uwepo wa bacteria wakati wa operesheni yanahusika na tofauti hii.

Akinamama wanaovuta sigara wakati wa ujauzito husababisha watoto wao tumboni kuwa na uwezo mdogo wa kupumua na kuongeza hatari ya watoto wao watakaozaliwa kupata pumu. Utafiti umeonyesha kuwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti) wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kuja kupata pumu baadaye.

5, Msongo Wa Mawazo:

 Kupatwa na (Msongo wa mawazo) mara kwa mara kunaongeza uwezekano wa kupata pumu, moja ya sababu ni tabia za mtu anapokuwa na msongo wa mawazo kama vile kuvuta sigara kunakochochewa na msongo wa mawazo. Maelezo ya hapa karibuni yanaonyesha kuwa mfumo wa kinga za mwili hubadilika mtu anapokuwa na msongo wa mawazo.

6. Urithi:

 Wazazi wanahusika katika kumfanya mtoto awe na pumu, inakadiriwa kuwa katika watoto watano wenye pumu, watatu huwa ni pumu za kurithi kutoka kwa wazazi wao.

Je,  pumu inatibika?
Pumu ni ugonjwa wa kudumu ambao haujapatiwa dawa ya kuuondoa moja kwa moja.

Tunapozungumzia tiba ya pumu tunamaanisha ushirikiano wa pamoja wa daktari na mgonjwa au na mzazi wa mtoto mgonjwa katika kuudhibiti ugonjwa huu ili:

  1. Kuzuia mgonjwa asirudiwe na matatizo ya mara kwa mara ya kukohoa, kubanwa pumzi na mengineyo yanayoambatana naugonjwa huu

  2. Kupunguza uwezekano wa kuzidiwa na kuhitaji huduma ya dharura

  3. Kuyaweka mapafu katika hali nzuri wakati wote

  4. Kumwezesha mgonjwa kushiriki katika shughuli za kawaida za kimaisha na kupata usingizi mzuri

  5. Kuzuia mgonjwa asibanwe na pumu na kusabibisha tiba za dharura


Mgonjwa anahitaji kuwa na mpango mzuri unaoelekeza namna ya kutumia dawa ipasavyo, namna ya kuzuia mgonjwa asikumbane na vitu vinavyochochea pumu (asthma triggers), namna ya kufuatilia jinsi mgonjwa alivyoweza kuudhibiti ugonjwa huu na namna ambavyo mgonjwa atakavyoweza kupata huduma ya dharura endapo atazidiwa.

Tiba ya pumu huwa inagawanywa kwenye makundi mawili; tiba ya kutoa msaada wa haraka na tiba ya muda mrefu ya kudhibiti pumu.

 Tiba ya kutoa msaada wa haraka ni ile inayotolewa pale mgonjwa anapoona dalili za kubanwa na  pumu,  na tiba ya muda mrefu ya kudhibiti pumu inalenga kupunguza athari zinazotokea kwenye njia za hewa na hivyo kuzuia kutokea kwa kubanwa na pumu.

Dawa za pumu huweza kutolewa kama vidonge, lakini nyingi huwa kama unga au mvuke ambavyo mgonjwa atavitumia kupitia kinywani mwake kwa kutumia kifaa kinachoitwa Inhaler. Inhaler ni kifaa kinachosaidia dawa kupita kirahisi katika njia za hewa kuelekea kwenye mapafu.

Tiba Ya Muda Mrefu Ya Kudhibiti Pumu
Watu wengi wenye pumu hutumia njia za muda mrefu za kudhibiti pumu kila siku ili kuzuia uwezekano wa kutokea matatizo yanayoambatana na ugonjwa huo.

Njia hizi za muda mrefu hupunguza kuathirika kwa njia za hewa (kuvimba kwa ndani na kuwa sikivu kuzidi kiwango) na hivyo kuondoa uwezekano wa kutokea kwa kubanwa na pumu. Njia hizi hazisaidii kutoa msaada wa haraka kwa mgonjwa.

Watu wengi wenye pumu hutumia corticosteroids ( inhaled corticosteroids ) kila siku ili kudhibiti ugonjwa wa pumu walio nao. Corticosteroids ni kundi la kemikali ambazo hutengenezwa na figo au kwenye maabara ambazo hufanya kazi nyingi mwilini ikiwa ni pamoja na kupunguza vimbe katika mwili.

Matumizi ya dawa hii yameonyesha kuwa bora katika kuzuia kutokea kwa uvimbe na athari nyingine kwenye njia za hewa zinazotokana na mtu kuvuta hewa yenye vitu visivyopendwa na mwili wa muathirika. Dawa hii hutumiwa kwa kuvutwa kwa mdomo kutoka kwenye kifaa maalumu.

Matumizi ya inhaled corticosteroids yana athari zake zikiwa ni pamoja na maambukizi ya mdomoni (thrush) yanayosabababishwa na matone ya dawa hiyo kuangukia kwenye mdomo au kooni. Dawa hiyo pia huweza kuathiri mboni za macho na kupunguza uimara wa mifupa endapo itatumika kwa muda mrefu.

Peak Flow Meter
Hiki ni kifaa kidogo cha kushikwa mkononi ambacho kinaonyesha jinsi hewa inavyotoka kutoka katika mapafu ya mtumiaji. Mtumiaji anapuliza kwa mdomo kwenye kifaa hicho na ataonyeshwa alama alizopata ( peak flow number) ambazo ni ishara ya ubora wa kiafya wa mapafu yake kwa wakati huo alipopuliza kwenye kifaa hicho.

 Mtumiaji anakitumia kifaa hicho kwa namna na muda alioshauriwa na daktari wake, kwa mfano, daktari anaweza kumshauri mgonjwa kukitumia kifaa hichio kila siku asubuhi na kunukuu alama anazopata kisha kumpelekea baada ya kipindi fulani ili aweze kushauriwa dawa za kuendelea kuzitumia.

Peak Flow Meter
Matumizi ya kifaa hiki yanaweza kukupa taarifa mapema ya hali ya kubanwa na pumu inayotegemea kukupata, ukajihami kwa kutumia dawa za kutoa msaada wa haraka na baadaye kujipima tena baadaye ili kuona msaada uliopewa na dawa ulizozitumia.

 

mzunguko.com

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload