AJIRA ZA AFYA ZASITISHWA

November 3, 2017

 

DAR ES SALAAM, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesitisha ajira mpya za kada ya afya zilizoombwa kwa kipindi cha Agosti mwaka huu. Taarifa iliyotolewa Oktoba 31 na Tamisemi ikieleza kusitisha ajira hizo kwa walioitwa kazini.

Taarifa hiyo iliwataarifu waajiri na waombaji wote wa nafasi za ajira za kada za afya kuwa imesitisha zoezi hilo kwa muda mfupi ili kukamilisha taratibu za ajira.

“Tafadhali  rejeeni tangazo letu lenye Kumb. Na CD. 162/355/01 la tarehe 30 Oktoba, 2017 lililowataarifu waombaji wa kazi wa nafasi mbalimbali za kada za afya. Walioomba kazi kuanzia 25/07 - 30/08/2017,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imethibitishwa kutolewa na Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Zainabu Chaula kuwa ni kweli wamesitisha kwa muda kwa sababu za kiufundi na halihusiani na madaktari wa Kenya.

Hivi karibuni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kwamba kumekuwa na upungufu wa watumishi wa afya hivyo wapo katika mikakati ya kuhakikisha wanaajiri upya watumishi.

Alisema kwamba wizara yake kupitia kibali cha Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, walitangaza nafasi za kazi 3,152 kwa wahitimu wa kada za afya nchini.

“Wizara ina jukumu la kuwapangia vituo vya kazi waombaji wenye sifa kwa mujibu wa waraka wa maendeleo ya utumishi namba moja wa mwaka 2009 kuhusu muundo wa utumishi ya kada ya chini ya wizara ya afya,” alisema waziri huyo.


MZUNGUKO.COM

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon