HATMA YA BARCA KATALONIA IKIJITOA HISPANIA.Klabu ya FC Barcelona imefahamika sana duniani kutokana na soka na imeonekana kuchukua msimamo katika mjadala kuhusu uhuru wa jimbo la Catalonia nchini Uhispania.

Bendera na rangi za klabu hiyo zimekuwa zikitumiwa katika maandamano ya kuunga mkono uhuru wa jimbo hilo - kupitia kura ya maoni ambayo ilikuwa imeharamishwa na mahakama ya Uhispania mjini Madrid.

Swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza ni hatima ya klabu hiyo ya jiji la Barcelona, jiji kubwa zaidi Catalonia, iwapo jimbo hilo litafanikiwa kujitenga.

Je, wataendelea kucheza La liga?

Mashabiki wataendelea kufurahia mechi za utani wa jadi za El Clásico kati ya Barça na mahasimu wao wakuu Real Madrid?

Katika mechi hizo, Real wanaongoza wakiwa na mechi 95 ambazo wameshindwa dhidi ya 91.

Wanaosimamia FC Barcelona wanasisitiza kwamba wao si wanasiasa; na kwamba rasmi klabu hiyo haina msimamo kuhusu uhuru wa jimbo hilo.

Aidha, hawajataka kujihusisha katika mjadala kuhusu ligi ambayow atashiriki Catalonia wakijiondoa kutoka Uhispania.Mwaka 2014 hata hivyo FC Barcelona walijiunga na Mwafaka wa Taifa wa Haki ya Kuamua, kundi lililojumuisha vyama vya kisiasa na mashirika ya kijamii ambayo yalikuwa yanaunga mkono kura ya maoni ya kujitenga kwa Catalonia.

Klabu hiyo, siku chache kabla ya kufanyika kwa kura hiyo baada ya polisi wa Uhispania kuanza kuwakamata maafisa wa serikali ya Catalonia, ilitoa taarifa ya kisiasa na kusema inatetea "demokrasia, uhuru wa kujieleza, na uhuru wa kuamua mustakabali wa taifa".

FC Barcelona wanaonekana kuamini kwamba wenyewe ndio wataamua ni ligi gani wataendelea kucheza.


Hata Catalonia ikijitenga kutoka kwa Catalonia, Barça wanaamini Wahispania hawataacha kutazama mechi za El Clásico.

"Tutasalia katika ligi moja na Espanyol," alisema naibu rais wa FC Barcelona Carles Villarubí mapema mwezi uliopita akizungumzia klabu ya pili kwa umaarufu zaidi mjini Barcelona, ambayo mashabiki wake wengi huunga mkono kusalia Uhispania.

Lakini Javier Tebas, rais wa shirikisho la Uhispania linaloandaa La Liga alijibu: "Barcelona hawawezi kuamua watachezea soka wapi iwapo shughuli ya uhuru itakamilishwa Catalonia."


FC Barcelona wameshinda mataji 24 ya La Liga, ikiwa ni pamoja na michuano ya kwanza 1929

  • Pia wameshinda vikombe 29 vya Copa del Rey, vikombe vingi zaidi ya klabu nyingine.

  • Kumechezwa mechi 235 rasmi kati ya Barcelona na Real Madrid, kuanzia kwa mechi ya kwanza ya Copa del Rey mwaka 1916. Real wameshinda mechi 95, Barça 91 na 46 zimeisha kwa sare.

Duru katika klabu hiyo zimeambia BBC kwamba hakutakuwa na taarifa zozote rasmi kwa sasa kuhusu hatima ya klabu hiyo.

Lakini duru hizo zinasema: "Iwapo Catalonia watafanikiwa kujitenga, klabu hiyo itahitajika kuzingatia maoni ya wanachama wake kabla ya kufanya uamuzi huo muhimu.

"Pili, na kwa heshima zote, tunaamini kwamba sisi ni nembo miongoni mwa zinazoongoza katika soka duniani na ligi yoyote ile inaweza kufurahia sana kuwa nasi, ikiwa ni pamoja na Ligi ya Uhispania."

Gabriel Rufián, mwanachama wa Chama cha Republican cha Mrengo wa Kushoto cha Catalonia amesema uwezekano wa Barça kuendelea kucheza ligi ya Uhispania hauwezi kuwa na tofauti yoyote na Monaco ambao hucheza Ligi Kuu ya Ufaransa ilhali nchi yao si sehemu ya Ufaransa.

Ni wachache sana ambao wako tayari kufikiria uwezekano wa kuwa na ligi kuu ya Catalonia ambayo bila shaka itatawaliwa na Barça iwapo itaundwa.


Uwezekano wa Lionel Messi kuwakabili mabeki wa klabu ambazo hazina uzoefu mkubwa katika ligi Catalonia, iwapo kutakuwa na ligi kama hiyo, haujawaingia vyema akilini watu wengi.

"Siwezi kufikiria La Liga ya Uhispania bila Barcelona," mkufunzi mkuu wa Real Madrid Zinedine Zidane anasema.

"Kama shabiki wa kandanda na michezo kwa jumla siwezi kulifikiria jambo kama hilo."


mzunguko.com


CHANZO:BBC


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu