BIMA YA AFYA KWA WATANZANIA WOTE.
Serikali imesema ili kukabiliana na ongezeko la gharama za matibabu kwa wananchi, imeandaa muswada wa bima ya afya kwa wote ambao utamfanya kila Mtanzania awe na uhakika wa matibabu. Hayo yalisema jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akizindua kongamano la 49 la afya, likiwa na ajenda ya kukuza maadili ya kitabibu na kitaaluma miongoni mwa wataalamu wa afya.

Kongamano hilo, lililofanyika Hoteli ya Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam, lilikwenda sambamba na Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat). Makamu wa Rais alisema Serikali inafanyia kazi mkakati huo mpya wa utoaji huduma za afya kwa mfumo wa bima na tayari inaangalia namna ya kutumia vyanzo vya ndani vya fedha kukamilisha lengo hilo. Alikuwa akijibu moja ya hoja zilizotolewa na rais wa Mat, Obadia Venance Nyongole katika hotuba yake. “Nimesikiliza kwa makini hotuba ya rais wenu na ninajua wengi mna shauku ya kupata majibu ya hoja hizo na nichukue fursa kuzijibu,” alisema Makamu wa Rais. Hoja ya madaktari hao ilikuwa ni kuishauri Serikali kuanzisha tozo maalumu kwenye bidhaa kama mafuta na madini ambazo zitachangia huduma za afya, hasa kufidia gharama za wagonjwa wanaotibiwa kwa msamaha na wenye mahitaji maalumu. “Ili kukabiliana na ongezeko la gharama za matibabu kwa wananchi, Serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwamo kuandaa muswada wa bima ya afya kwa wote ambao utamlazimu kila Mtanzania kuwa mwanachama,” alisema Samia. “Hii itamuondolea usumbufu wa kutopata matibabu pindi anapokuwa anahitaji.” Kwa sasa huduma ya bima ya afya inatolewa kwa mtu anayejiunga kwa hiari, na ingawa mwitikio umekuwa mkubwa, wananchi wengi hawajajiunga na huduma hiyo. Lakini Serikali imeshaanza kutoa vitambulisho kwa wazee ili wapate matibabu bure. “Serikali itaendelea kuchukua hatua za makusudi za kuwatambua wazee wasiojiweza, wenye umri wa miaka 60 na zaidi katika kila halmashauri kote nchini ili wapatiwe vitambulisho vitakavyowawezesha kupata huduma za afya bila ya malipo,” alisema Mama Samia. “Vilevile, kwa mujibu wa sera, tunayo makundi maalumu; mfano watoto chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito ambao wanatakiwa kupata matibabu bila ya malipo.” Awali rais wa Mat alisema iwapo Serikali itafanya mabadiliko ya kimfumo, itachangia ongezeko la fedha za maendeleo kwenye sekta ya afya ili kufanya hospitali na vituo vya umma kujiendesha kwa faida na hilo pia litafanikiwa iwapo kila Mtanzania atakuwa na bima ya afya.“Iwapo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) utalipa kutokana na gharama halisi za matibabu kwenye soko na kwa wakati tutafanikiwa hili. Lakini tunashauri Serikali ianzishe tozo maalumu kwenye bidhaa kama sigara, mafuta na madini ambazo zitachangia huduma za afya nchini kufidia gharama za wagonjwa wanaotibiwa kwa msamaha,” alisema. Wakati huohuo, Makamu wa Rais alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuanzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo ya udaktari ili kuwapunguzia mzigo wa mikopo wanayokabiliana nayo wanapoanza ajira. Alisema kwa kuwa wanafunzi wa udaktari wanatumia muda mrefu katika masomo, huhangaika kulipa mikopo badala ya kujikita kwenye kazi, hivyo ufadhili utawaondolea hali hiyo. “Acha niwamegee siri, kwa sasa Serikali inafikiria namna ya kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea fani ya udaktari kwa kuwa wanasoma taaluma hiyo kwa muda mrefu na wana jukumu kubwa la kuhudumia jamii,” alisema Samia. Aliongeza kuwa anaamini ufadhili huo utawavutia zaidi vijana kuchagua fani ya udaktari na kuongeza ari ya utendaji kazi. “Niwahakikishie kuwa tunatambua kuwa tunatakiwa kuboresha zaidi masilahi yenu, kama tayari tumeshachukua hatua za kuongeza viwango mnavyolipwa kwa kumuona mgonjwa NHIF niseme kuwa tutalipa uzito suala hili na kuzingatia mara uwezekano ukipatikana,” alisema. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kupandisha bajeti ya sekta ya afya kutoka asilimia 9.2 mwaka 2015/16 mpaka asilimia 10.1 mwaka 2017/18.


mzunguko.com


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu