FAHAMU KWANINI WASOMI WENGI KUKOSA AJIRA?
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi wa kitanzani na hili limeshuhudiwa zaidi katika majaribio mbalimbali ya nafasi za kazi ambapo vijana wengi hujitokeza kuomba ajira,.Ikumbukwe adha hii ya ajira sio tu kwa vijana wadogo bali kwa watu wenye umri zaidi ya vijana ambao wengi wao ni walioacha kazi zao za awali au kuzipoteza kutokana na mambo mbalimbali yatokeayo kwenye mazingira ya kazi zilizopita.


Tanzania ni moja kati ya nchi yenye tatizo la upungufu mkubwa wa ajira na ndio maana Raisi wa awamu ya tano Mh Dr John Pombe Magufuli akaamua kuja na kauli mbiu ya Tanzania ya viwanda ili kutengeneza nafasi nyingi za ajira haswaa kwa vijana wa kitanzania.

Lakini bado tatizo hili limezidi kuwa kubwa sana kwa kuwa wahitimu wanaomaliza vyuo kuongezeka kila mwaka na kukutana na wengine ambao sio wahitimu wa vyuo vikuu na wahitimu waliomaliza masomo yao miaka iliyopita bado wako mtaani,kwa mfano wahitimu wa shahada ya ualimu wako mtaani tangu mwaka 2014 mpaka leo hawajaajiriwa na bado serikali haina mpango huo hasa kwa masomo ya sanaa ambao idadi yao ni kubwa sana.


Mpenzi msomaji wa makala hii ya leo lazima tujiulize kwanini kuna rundo la wahitimu wa vyuo vikuu mtaani, kwa idadi kubwa hiyo huku wengi wakiishia kufanya majaribio ya kazi bila kuajiriwa, mbaya zaidi kushindwa kujiajiri kabisa?


Je Kwanini wahitimu wengi hukosa ajira?


1:UFINYU WA NAFASI ZA AJIRA SERIKALINI.

Hakika hapa kila msomi atakuwa anaelewa nataka kuzungumzia nini,lakini ni wazi na dhahiri kuwa serkali bado inatoa nafasi chache sana za ajira kulinganisha na wanaomaliza katika taaluma mbalimbamli ambao wanahitajika na serikali,siamini kama walimu wa sanaa katika shule zetu nchini wameajaa na wametosha kwani hata maeneo ya mjini kwa sasa kuna shule ambazo mwalimu mmoja anahudumia idadi kubwa sana ya wanafunzi kwa darasa moja,kwani kitaalamu mwalimu mmoja ni vizuri akahudumia wanafunzi wasiozidi 50 kwa darasa moja ila bado haipo hivyo,kwa hiyo ni vizuri kama serikali zetu zingeangalia upya utaratibu wa utoaji upya wa ajira.


2:UBOVU WA MITAALA YA ELIMU ITOLEWAYO.

Hakika acha niliseme hili na kila mtu asome na asikie,mitaala yetu ya elimu bado ni changamoto katika soko la ajira kwani haimpi mwanafunzi mbinu za kujikwamua kiuchumi bali zinamuandaa mwanafunzi kuja kuwa mtumishi mwadilifu kwa bosi wake,mitaala bado haijabadilika kulingana na wakati uliopo sasa wa DUNIA YA SAYANSI YA MAWASILIANO,ambapo kutengeneza pesa hakuhitaji mtu kuwa na shamba kubwa sana au kumiliki mifugo mingi sana kama kigezo cha utajiri kwani biashara za mitandao zimekuwa chachu kubwa sana ya mabadiliko ya uchumi,hivyo mitaala yetu ni bora ingeangaliwa upya kulingana na nyakati mpya za sasa.


3:MFUMO WA KUFAHAMIANA BADO UNASUMBUA WENGI.

Hii nayo ni changamoto katika soko la ajira kwani watu wengi husumbuka sana kupata ajira kama ni mtoto wa mvuja jasho kutoka Kata ya kaloleni,Njoro au Kahe na huna yoyote anaemfahamu kumshika mkono hakika atasota,kwani ni mara kadhaa nimeshuhudia waajiri wakisema ni ngumu kumuajiri usiemjua na kumuacha unaemjua,kuna wakati nilifanya jaribio mahala fulani lakini sikupata nafasi kwa kuwa aliyekuwa anaajiri alisema alikua anafata protokali za kufanya jaribio hilo hivyo atakaowaajiri anawajua,niliumia sana kwa kuwa nilikuwa nimewazidi kila kitu ila mbaya ni kwamba nilikuwa sina ninaemfahamu kunisaidia kuipata ajira ile.


4:MAWAZO FINYU YA WASOMI WENGI.

Katika kipindi amabacho wasomi wengi kuonekana kuwa hawana jipya ni hichi,kwani kuna wakati huwezi kutofautisha wazo la msomi na asie msomi,kuna wakati ukaona ni bora kukaa na asie msomi atakusaidia mawazo ya maisha kuko kukaa na wasomi wanaowaza mambo yasiyojenga,mfano unakuta msomi wa chuo anawazahuwezi kufanikiwa bila kujiunga freemason, mpaka unashangaa hii ni nini lakini hakuna cha ajabu kwa kuwa mawzo yetu wasomi kuna wakati bado ni mgando sana,lazima tufahamu huwezi kufanikiwa bila kutaabika na kuhangaika pasipo kukata tamaa,kwani kufanikiwa sio tambarare kama unavyodhania.


5:MAWAZO FINYU YA WAAJIRI.

Hili pia limekuwa tatizo kubwa kwa waajiri wengi,Lazima ieleweke kwamba Tanzania sio nchi inayotumia lugha ya kingereza hivyo ni swala la kawaida kumuona msomi akimaliza shahada na klugha ya kingereza kwake ikawa sio nzuri sana,hasa kwa wale waliotoka shule za kata kama mimi na wewe na nyinginezo ambazo mpaka mwalimu aongee kiswahili ndo aeleweke bila hivyo darasa zima watafeli na mwalimu atafukuzwa,kuna wakati una ujuzi mkubwa sana la ari ya kujituma ila lugha sio nzuri sana na utakosa ajira kwa kuwa muajiri amemsikia mwingine akiongea kingereza kizuri zaidi yako na kuvutiwa na lugha na wala sio utendaji.

Makamu mkuu wa Chuo Kikuu Dar es salaam Profesa Rwekaza Mukandala alisema kwamba"BAADHI YA WAAJIRI WANACHANGANYA KATI YA UJUZI NA LAFUDHI"hivyo kubabaika na wanaotoka nje ya nchi wakidhani ni bora kwa kuwa huongea lugha ya kingereza kwa lafudhi safi na kwa ufasaha sana, hivyo wahitimu wa ndani kunyimwa ajira kwa sababu zisizo na mashiko yoyote.


6:KUCHAGUA KAZI KWA WASOMI WENGI.

Ni dahahiri wasomi wengi huwa na mawazo makubwa wawapo masomoni lakini mambo huwa tofauti wamalizapo masomo yao kwani mtaani mambo ni tofauti sana na waliyokuwa wanayawaza wakiwa vyuoni,wasomi wengi huwaza kuwa mameneja au wakurugenzi na kadhalika lakini mambo huwa sio hivyo kwani ni wachache sana ambao mambo huenda kama walivyopanga,hivyo wakikuta mambo sio hawataki kufanya kazi nyingine yoyote wakisubiri kuwa mameneja na nyadhifa nyingine nzuri walizoziota awali.


7:KUBWETEKA

Kuna wasomi mpaka leo wanasubiria kazi zitolewe na serikali na waajiriwe,lakini bado hakuna uhakika wa kazi hizo,hivyo kuendelea kuongeza idadi ya rundo la wasomi wasio na ajira mtaani,vijana lazima wajiongeze kufanya mambo mbalimbali hata kama hukusmea hicho usibweteke kijaribu huenda ndio kitakachokupa ajira ya kudumu na kukuondoa kwenye baa la ukosefu wa ajira.Kwa mfano wapo wengi ambao ni wafanyakazi wa kampuni mbalimbali hawakusomea lakini wanafanya tena kwa mafanikio makubwa,cha msingi ni kujituma na kuwa na ari ya kujifunza kwani Dunia imebadilika sio lazima uwe mwalimu kwa kuwa umesomea ualimu unaweza ukawa hata Mshauri wa maswala ya ukimwi au mjasiriamali na ukafanikiwa.


Mwisho nipende kuwashukuru wote mtaopitia makala yangu hii,ni vyema tukaenda nawakati na tukumbuke hii ni dunia nyingine sio ilee ya miaka ile lakini bado tuna nafasi ya kujifunza na kuchukua maamuzi mapya ya kujenga maisha yet na tuache kulalamika na kuilamu serikali kila siku tushachelewa haitatusaidia chochote bali tujipambanue kwa mapana zaidi.Nakumbuka kuna wakati nilikuwa boda boda na sikukata tamaa nilipambna japo nilipata changamoto kubwa ila unajifunza kupitia pale ili siku ukifanikiwa uheshimu mafanikio yako na wengine wanufaike.Imeandikwa na Sam Kameme.

mzunguko.comTufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu