IDADI YA WALIOUAWA SOMALIA YAONGEZEKA.

Mogadishu, Somalia. Idadi ya watu waliouawa katika mlipuko mkubwa wa bomu Jumamosi iliyopita katika eneo lenye shughuli nyingi za kibiashara mjini hapa imefikia watu 300 huku wengine 300 wakiwa majeruhi. Rais Mohamed Abdullahi "Farmajo" Mohamed alilaumu kundi la al-Shabab lenye mafungamano na al-Qaeda kwa kuhusika na shambulizi hilo baya zaidi kutokea nchini tangu kundi la al-Shabab lilipoanzisha harakati zake mwaka 2007. "Tumethibitisha kuwa watu 300 waliuawa kwenye mlipuko huo. Idadi ya watu waliokufa huenda bado ikaongezeka kwa kuwa bado wengi hawajulikani waliko," Abdikadir Abdirahman, mkurugenzi wa idara ya magari ya kusafirisha wagonjwa aliliambia shiria la Reuters. Mashirika ya habari ya kimataifa yameripoti kuwa mkasa huo ulitokea wakati lori lililokuwa limejazwa milipuko lilipolipuka karibu na lango la hoteli.


Shirika la habari la Reuters lilimnukuu Ahmed Ali, muuguzi anayefanya kazi kwenye hospitali moja akisema kuwa miili 160 haikuweza kutambuliwa kwa kuwa ilichomeka vibaya hivyo ilizikwa na serikali jana na miili mingine iliziwa na jamaa zao. Wafanyakazi wa idara ya afya wanahangaika kutambua na kutibu majeruhi wa shambulizi hilo la kikatili zaidi kwani watu 100 hawajulini walipo.

Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezekana kwani wengi inaaminika wamefukiwa kwenye vifusi vya jingo hilo lililoharibiwa. "Tunatarajia idadi ya vifo itaongezeka," alisema Abdirahman Omar Osman akiongeza kwamba wafanyakazi wa uokozi wanahitaji msaada kwa sababu vifaa walivyonavyo haviwezi kuondoa kifusi. "Bado tunaendelea kukusanya habari kutoka hospitali mbalimbali na ndugu wa marehemu. Wengine wamefikishwa hospitani wakiwa na majeraka makubwa. Pia tumearifiwa kuna ndugu wengine wanawaondoa hospitalini jamaa zao majeruhi,” aliongeza. "Baadhi ya majeruhi wanahitaji uangalizi maalumu kwa vile hawawezi kutibiwa hapa. Wengi watasafirishwa leo kwenda Uturuki baada ya kuitikia ombi letu la msaada," alisema Osman. Alisema timu ya madaktari kutoka Uturuki ikiongozwa na Waziri wa Afya, Ahmet Demircan wamewasili leo asubuhi mjini Mogadishu kwa ajili ya kusaidia kusafirisha watu zaidi ya 70 wanaohitaji matibabu ya ziada. Chanzo: Mwananchi


Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Jiunge nasi :

Usipitwe na kitu