MZALENDO WA KWELI LAZIMA ALIPE KODI

June 14, 2017

 

 

 

 

Katika nchi zinazoendelea, Serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha maendeleo ya wananchi

 

yanapatikana. Kwakuwa nchi nyingi zinazoendelea hazina rasilimali zakutosha au hazitumii rasilimali

 

zao kwa ufanisi kamili, na pia sekta binafsi katika nchi hizi hazina nguvu sana na nyingi zinajali zaidi

 

faida zao wenyewe kuliko faida za jamii nzima, ni muhimu na jambo la kizalendo kwa serikali

 

kukusanya kodi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.

 

     Katika Makala hii, tunajadili umuhimu wa ulipaji kodi na faida gani nchi inapata kwakuwa na

 

mfumo mzuri wa ulipaji kodi.

 

 

 

Faida za ulipaji Kodi: 

 

 

1.    Kwanza kabisa, kodi husaidia serikali kutoa huduma za kijamii kwa jamii inayoiongoza. Kodi

 

inawezesha serikali kujenga shule, zahanati, kutoa maji safi na huduma nyingine ambazo jamii 
 

inahitaji. Huduma hizi zinaleta faida kwa jamii nzima na si kwa mtu mmoja mmoja.

 

 

2.    Pia, Kodi husaidia serikali kujenga na kuendeleza miundombinu katika nchi. Kodi huipatia

 

serikali fedha ya kujenga miundombinu kama barabara, reli, madaraja, vivuko n.k. vyote hivi

 

vinajengwa kwa faida ya wananchi wote.

 

 

3.    Kodi husaidia kuboresha usawa wa kipato baina ya wananchi katika nchi. Baadhi ya mifumo ya

 

kodi inaangalia mtu au biashara inapata kipato gani na hivyo huwatoza kodi kutokana na kipato

 

wanachopata. Hivyo, anaepata kipato kikubwa anatozwa kuliko anaepata kipato kidogo na matokeo

 

yake kunaongeza usawa wa kiuchumi baina ya watu katika jamii.

 

 


4.    Kodi husaidia pia kuhakikisha soko la nchi linafanya kazi kwa ufasaha. Kwa kuhakikisha kuna

 

mazingira mazuri ya biashara na kuhakikisha mali za watu zinalindwa, na kuweka sharia nzuri za

 

biashara zinazomlinda mteja na kumvutia mwekezaji.

 

 

5.    Kodi inawezeha watu, biashara na wakazi kufanya vitu vya kimaendeleo kwa pamoja ambapo

 

vitu hivi visingewezekana kwa mtu kufanya kivyakevyake. Kama msemo wa kiswahili usemavyo,

 

"umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu." Mapato ya kodi yanaonesha umoja wetu katika kuiendeleza

 

nchi.
 

 

 

    Hizi ni baadhi tu za faida za ulipaji kodi. Vizazi vilivyopita vililipa kodi iliyosababisha maendeleo

 

tunayoyaona sasaivi na ni jukumu la kizazi hiki kulipa kodi ili kuendeleza maendeleo haya na

 

kuhakikisha watoto na wajukuu wetu wanakuta maendeleo katika nchi yetu. Kama Oliver Wendell

 

Holmes, Jr , mwanasheria alieitumikia Mahakama Kuu ya Marekani kuanzia mwaka 1902 mpaka

 

1931, alivyosema , “Kodi ndio bei tunayoilipa kwaajili ya ustaarabu.” Na mimi pia namuunga mkono

 

kuwa kodi ndio bei tunayoilipia kwa mapenzi yetu ya dhati ya nchi yetu nzuri Tanzania.

 

 

     Kwa kuzingatia haya, ni wazi kuwa mzalendo wa kweli anaeipenda nchi yake kwa dhati na sio

 

kinafiki, lazima ataona ni jukumu lake kulipa kodi na atalipa kodi bila shuruti. Lakini pia, mzalendo

 

huyu ana haki yakuuliza kodi yake inafanya nini. Watu wengi barani Afrika hawapendi kulipa kodi

 

kwasababu kwa miaka mingi kodi inayolipwa haitumiki vizuri. Mtu anadaiwa kodi nyingi lakini haoni

 

maendeleo katika jamii. Hii ni changamoto ambayo serikali lazima iifanyie kazi. Mimi binafsi

 

ninapolipa kodi, nategemea kuona maendeleo kutokana na kodi yangu ninayoilipa. Serikali ambayo

 

inakusanya kodi na kufanya mambo ambayo hayamsaidii mwananchi kwa kuleta maendeleo na

 

serikali inayoibia wananchi wake na haipaswi kuungwa mkono.

 

 

PENDA NCHI YAKO, LIPA KODI

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload

Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon