Tufuate kupitia:
  • YouTube Social  Icon
  • Twitter Social Icon
  • Black Instagram Icon
  • Facebook Social Icon

Faida ya Elimu katika Nchi

January 23, 2017

 

 

 

Kusema kweli, kuna sababu moja tu inayozifanya nchi change kama zetu zijenge na kuendesha vyuo vikuu. Tunaweka rasilmali kwa manufaa ya baadaye. Tunatumia fedha nyingi sana zisizolingana na uwezo wetu kuwasomesha watu wachache, ili baadaye na wao walete faida kubwa kiasi hicho hicho katika nchi. Tunatumia fedha kutafuta faida katika akili ya mwanadamu, kama vile vile tunavyotumia fedha kununua trekta. Na kama vile vile ambavyo tukinunua trekta tunalitajia kufanya kazi kubwa zaidi kuliko kazi ya mtu na jembe lake la mkono, vile vile tunatarajia mwanafunzi tuliyemsomesha Chuo Kikuu kutusaidia kiasi kikubwa zaidi katika kazi za maendeleo yetu kuliko yule ambaye hakupata bahati hiyo. Tunatoa vingi kumpa mwanafunzi wakati akiwa katika Chuo Kikuu, ili baadaye tuweze kupokea vingi zaidi kutoka kwake. Hakuna upendeleo wowote katika jambo hili; watu maskini hawana fedha za kupendeleana. TUNAYO HAKI YA KUTAZAMIA MATUNDA KUTOKA KWA WALE WALIOHITIMU KATIKA CHUO KIKUU, NA WENGINE WALIOPATA ELIMU YA JUU YA AINA YO YOTE; HATUNA MATUMAINI MATUPU, TUNATAZAMIA KUVUNA.

                Si jambo la ajabu, Mheshimiwa Rais, nchi kuwa na lengo kama hilo, wala si madai ya pekee ya Waafrika Fulani kwa Waafrika wenzao, ambayo hayatolewi katika sehemu nyingine duniani. Unafahamu zaidi kuliko mimi, kwamba miaka elfu mbili iliyopita, Bwana Yesu alisema, “Na kila aliyepewa mengi;naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watamdai zaidi”. Tunadai nini basi kwa wale wenzetu waliojaliwa kupata elimu? Tunadai huduma kwa wananchi, na huduma ambayo ukubwa wake utalingana na kiasi cha elimu waliyoipata.

                Ni Dhahiri kwamba mtu anaweza kuitumia elimu aliyoipata shuleni au katika chuo kwa faida yake mwenyewe binafsi, na faida nyingine kwa wananchi zikapatikana kwa bahati tu. Na kwa kweli  wakati mwingine inaonekana kwamba utaratibu wan chi zetu ndivyo ulivyo, kwa sababu vishawishi vya mishahara ya juu vimewekwa kwa zile kazi ambazo hazina faida kubwa kwa wananchi kwa jumla. Lakini, hata katika zile kazi za kuwahudumia sana wananchi, mara nyingi watu wenye elimu au utaalamu wanaweza kutumia vibaya dhamana yao, wakipenda. Watu wamepata kudai mishahara minene zaidi, au masharti bora zaidi ya kazi, kwa kutumia utaalamu na ujuzi walioupata kwa gharama ya wananchi. Badala ya kukubali kwamba wanadaiwa kulipa huduma kwa wananchi, watu hawa wanadai tena mapato makubwa, ili tofauti yao na wafanyakazi wengine iwe kubwa zaidi na zaidi, kwa kisingizio kwamba wao ni muhimu sana katika kazi hizo: eti bila ya injinia daraja haliwezi kujengeka, n.k.

                Si nafasi yangu leo kusema, hata kwa nadharia, kama mawazo kama hayo ni sawa au si sawa. Sijui kama kweli injinia anastahili kupata pato kubwa zaidi kuliko fundi, au fundi zaidi ya kibarua; au hata kama Rais anastahili kupata pato kubwa zaidi kuliko watu waliomchagua. Lakini sisi tuliojaliwa kupata elimu tutaendelea kudai mapato makubwa zaidi kuliko yale tuliyokwisha kujipangia. Ni kweli kwamba daraja haliwezi kujengwa bila ya injinia; lakini vile vile haliwezi kujengwa bila ya vibarua. Je, inafaa siku zote kulinganisha mishahara yetu na ile minene zaidi wanayopokea watu wengine ambao pengine wamo katika nchi zizlizo tajiri zaidi kama vile Marekani na Ulaya, au tuanza sasa kuilinganisha mishahara yetu na ile ya wenzetu wenye kipato kidogo sana  kwa kufanya kazi ngumu sana, hata kama ni kazi ya aina nyingine? Yaani, ni haki kweli kutumia utaalamu ambao wananchi wametuwezesha kuupata, kuwa kama silaha ya kuwatishia wananchi wale wale?

                Kama tukikaa na kufikiri nafasi yetu ilivyo katika nchi zetu, nadhani hatutakubali kufanya hivyo. Maana kweli  ni kwamba, pamoja na kushika madaraka makubwa kwa sababu ya rasilmali iliyotumiwa kutuelimisha, tunazo vile vile nafasi nyingi za kujiendeleza- jambo ambalo linazidi kutambuliwa. Kuishi katika bara la Afrika leo ni nafasi inayofurahisha sana. Maendeleo ya Afrika ni nafasi pekee ya mtu kutumia akili yake, na tunayo nafasi ya kupanga na kuongoza matokeo ya kazi kama hizo. Tukichukua mfano ule wa daraja; kazi ile ya kubeba mifuko ya saruji, au kufanya kazi katika maji, na kadhalika, bila ya kujua  kazi hiyo hatima yake ni nini, si kazi inayofurahisha sana. Lakini inasisimua sana kushiriki katika kazi ya kuchora ramani ya daraja, na kushiriki tena katika kulijenga daraja hilo kwa kufuata ramani uliyoichora.

                Watu wenye shahada katika nchi zilizoendelea hawanazo nafasi kama hizo, kama tulivyonazo sisi katika Afrika; wala hawawezi kuwa na ridhaa ya moyoni kama tunavyoweza kuwa nayo sisi. Kijana wa kike au wa kiume katika Afrika anaweza kuwa na hakika ya kushiriki katika kuinua hali ya maisha ya wananchi katika taifa lake. Lakini anaweza akagundua kwamba kushiriki kwenyewe kunasaidia tu kuleta tofauti baina ya kionambali cha rangi na kile kinachoonyesha picha nyeusi na nyeupe, ambazo shabaha yake pengine hata siyo kusisimua mawazo ya wananchi. Lakini hata hivyo bado katika Afrika tunaweza, kwa kutumia ujuzi wetu, kuwasaidia wananchi kuleta mapinduzi katika maisha yao yaliyo ya kimaskini sana: yaani kutoka katika hofu ya njaa na shida daima, kufikia katika maisha yanayomstahili binadamu, na yenye raha kidogo. Tunaweza kuwapunguzia akina mama mzigo wao wa kujitwika mitungi ya maji mwendo wa maili nyingi; tunaweza kuwapatia mwanga na matumaini watoto wadogo ambao bila msaada huo watavia kwa kukosa chakula bora na maradhi. Tunaweza kugeuza nyumba zetu wenyewe, yaani aina ile ya nyumba ambamo wananchi walio wengi wanaishi, zikawa nyumba bora na mahali pa raha pa kuishi, ambapo kila mmoja ataweza kuishi kwa heshima.

                Lakini, kama tunataka kuifikia sifa hiyo ya kufanya kazi nzuri tukaridhika, basi kuna kipimo kimoja lazima tukifikirie. Sisi wenyewe lazima tuwe sehemu ya taifa hilo tunalotaka kulibadili. Hatuna budi kufanya kazi zetu kwa kushirikiana na wananchi wenyewe; siyo kuteremka tu, kama miungu ya kale, kufanya kitu siku moja, na halafu kutoweka tena. Nchi au kijiji, au kundi la watu, haliwezi kuendelezwa; watu wanaweza tu kujiendeleza wenyewe. Maana maendeleo ya kweli maana yake ni maendeleo ya watu. Kila nchi katika Afika inaweza ikaonyesha mifano ya maendeleo ya kisasa yaliyo vyombo au majengo ya kisasa waliyojengewa wananchi, na ambayo sasa yanaoza bila kutumika. Tunayo majengo ya shule, mifereji ya kumwagilia maji mashamba, majengo ya masomo yaliyo ghali sana, na kadhalika – vitu ambavyo mtu Fulani alikuja na kajaribu kuwaletea wananchi. Maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila wananchi wenyewe kushiriki. Watu wenye elimu wanaweza wakajitokeza kuongoza, na wanapaswa kufanya hivyo. Wanaweza wakaonyesha mambo yanayowezekana kufanywa, na jinsi yanavyoweza kufanyika. Lakini wanaweza tu kufanikiwa kuleta mapinduzi kwa watu kama watafanya kazi zao pamoja na wananchi. Ndiyo kusema kwamba watu wenye elimu wanaweza tu kuwa na faida kama watachanganyika kabisa na kuwa sehemu ya jamii wanayotaka kuisaidia: washiriki katika mafanikio na katika shida, na kujitumbukiza kabisa kwa lo lote litakalotokea.

                Ili waweze kufanya hivyo itawabidi waafrika wenye elimu wachanganyike kabisa na wenzao wasiokuwa na bahati ya kuwa na elimu, na wafanye hivyo bila kusitasita. La sivyo juhudi zao zitapotea bure. Katika Tanzania tumeyaona hayo kwa vitendo. Tumeona kwamba ukitaka kuleta mabadiliko ya haraka kijijini, si lazima kumtumia mtu mwenye elimu ya juu kuliko wote, au hata kiongozi wa Chama au Serikali. Unamtafuta mtu ambaye wananchi wa kijiji kile wanamheshimu na kumtambua kuwa ni kiongozi. Kama kiongozi huyu anayekubalika na wananchi ni mtu mwenye elimu, basi  maendeleo huwa mazuri zaidi nay a haraka zaidi, maana anaweza kuwaongoza kwa mioyo na kwa mawazo pia, na wakati huo huo wananchi wanamwona kuwa yeye ni mmoja wao. Kama mtu huyo hakupatikana, basi wa pili anayefaa ni huyu mwenye elimu anayesema vizuri na yule kiongozi anayekubalika katika sehemu ile. Hivyo anaweza kutumia ujuzi wake na kuleta maendeleo. Lakini kama huyu kijana mwenye elimu ana majivuno kwa sababu ya ujuzi wake, au yuko mbali sana na wananchi wengine kwa namna anavyoishi, hata wananchi wengine ama wamwogope ama wamdharau, ingekuwa bora zaidi kama kijana huyo asingalikuwapo kabisa, kwa sababu atasimamisha badala ya kusukuma mbele maendeleo.

                Lakini kusema hivyo maana yake si kusema kwamba mwalimu, au mtu yeyote mwenye shahada ya Chuo Kikuu, akitaka kufanikiwa katika kazi yoyote ya kuleta maendeleo ya taifa, basi lazima wakati wote aishi kama alivyoishi babu yake, bila ya kutumia ujuzi wake ulio mkubwa zaidi kujipatia maisha bora zaidi. Wala maana yake siyo kwamba huyu mwenye elimu lazima wakati wote akubali mawazo ya wananchi walio wengi. Lakini hitilafu zake za mawazo na wale wenzake lazima ziwe katika mabadiliko ya vitu ambavyo wananchi wale tayari wanavielewa. Tofauti hizo zisiachwe zikaonekana kuwa ni dharau ya wananchi walio wengi kwasababu ya hali yao ya maisha; lazima ziwe na msingi wa kuheshimu shida na mawazo ya wananchi. Na inapotokea kwamba huyu mwenye elimu ana maisha yaliyo tofauti kutokana na ujuzi wake ulio mkubwa zaidi, basi lazima awe tayari kuwaeleza tofauti hizo wale anaoishi nao na kufanya kazi nao, yaani akiwaona kuwa sawa na yeye. Kwa mfano, kama anachemsha maji kabla ya kuyanywa, na wenzake wakaona kuwa mtoto wake anayo afya bora zaidi, basi lazima awaeleze wenzake akiulizwa au nafasi ikipatikana, tofauti baina ya kunywa maji yaliyochemshwa na maji yasiyachemshwa. Na atafanya hivyo akitambua kwamba mara ya kwanza pengine wananchi hawatamwamini, na bila ya kuonyesha kuwa hao anaowaeleza ni wajinga wasiojua hata jinsi ya kutunza watoto wao.

                Maana ni jambo muhimu watu kukubali usawa bila ya kujali elimu waliyoipata. Na kwa kweli tutakuwa tunadhihirisha ujinga wetu sisi wenyewe tukidhani kuwa elimu na ufundi wa kisasa una faida, au tumenarikiwa kuupewa, kwasababu sisi ni bora kuliko wenzetu wasiopata bahati ya kupata elimu tuliyoipata. Jadi ya Kiafrika ya kuheshimu wazee haikuwa ya kijinga, wala si ya kijinga mpaka sasa. Tabia hiyo inatokana na watu kukubali kujifunza kutoka kwa wazee wao waliopata kuona maisha marefu zaidi na matatizo mengi zaidi. Mawazo ya kudhani kuwa wazee wa kijijini hawanalo lo lote walijualo kwasababu hawakupata elimu ni mawazo ya kijinga na yanaweza kuleta hasara kubwa. Kwa mfano, katika Tanzania bara wakoloni walimwaga shilingi milioni 720 kulima karanaga – lakini leo bado tunaagiza mafuta ya karanga kutoka katika nchi za nje. Moja ya sababu ya hasara hiyo kubwa ni kwamba mabingwa, yaani wale watu wenye elimu, walifanya hesabu ya wastani wa mvua katika kipindi cha miaka 10 katika sehemu ile, basi wakatayarisha mpango wao. Walifikiri kwamba, kwasababu wakulima wa sehemu ile walikuwa hawakupata elimu, wasingeweza hata kidogo kutoa habari zozote za mvua za sehemu ile: mwaka hata mwaka, au mwezi hata mwezi. Vile vile walidhani kuwa wanachi walikuwa wavivu tu walipoacha wasikate miti yote walipolima shamba. Kwa hiyo wakalima mashamba makubwa sana, na wakavuna karanga kidogo sana; lakini mmomonyoko wa udongo ukaanza!

                Sikuutoa mfano huo kwa nia ya kushutumu mabingwa wa kutoka katika nchi za nje. Ingeweza kupatikana mifano mingine ya mpango kushindwa kwasababu ya mawazo ya mabingwa wanachi. Nautoa mfano huo tu kwasababu umetuonyesha kosa lililotugharimu fedha nyingi kuliko kosa jingine lolote katika Tanzania, na linamfanya mtu atambue kwamba wote tunapaswa kujifunza kutoka kwa kila mtu. Ujuzi haupatikana katika vitabu tu, au kutokana  na hotuba za wataalamu, au kutoka kwa Marais wanaotutembelea. Tunayo hekima nyingi kutokana na maisha yetu ya zamani, na kutoka kwa wazee ambao bado wanao ujuzi walioulimbikiza katika jadi za makabila. Na hasa lazima tukumbuke kwamba ingawa huko nyuma Afrika ilikuwa nyuma kwa mambo ya ufundi, lakini haiwezi kuhesabiwa kuwa ilikuwa nyuma katika uhusiano iliyoujenga baina ya mwanadamu na mazingira yake. Tutakuwa wapumbavu sana tukiacha maendeleo ya uchumi wetu yaharibu desturi na mila ambazo makabila ya kiafrika yamezijenga kwa muda wa miaka mingi. Lakini tukitaka hizo zisiharibike, basi tusikubali kutawaliwa na kiburi na majivuno tunayoshawishiwa kuyajenga kwasababu ya elimu yetu.

                Mheshimiwa Rais. Ninalojaribu kusema ni kwamba sisi wote, wenye elimu na wasio na elimu, tu watu wa taifa moja, nasi tu sawa katika taifa hilo. Tunaweza kujaribu kujitenga na wenzetu kwasababu ya elimu yetu tuliyoipata; tunaweza tukajimegea sehemu kubwa zaidi kutokana na mapato ya taifa letu. Lakini gharama ya kufanya hivyo, kwetu sisi wenyewe na kwa wananchi wenzetu, itakuwa kubwa sana. Itakuwa kubwa si kwasababu ya kupungukiwa maendeleo yet utu, lakini vile vile  kwasababu ya kuhatarisha usalama wetu na maisha yetu.

                Lakini maneno hayo maana yake ni kwamba mafunzo ya chuo kikuu, na chuo kikuu chenyewe, yanaweza yakastahili tu katika Afrika kama mafunzo hayo, na chuo hicho, shabaha yake ni kutimiza mahitaji ya wananchi, ambao wengi sana hawakupata nafasi ya elimu. Kwa hiyo lazima chuo kikuu kiwe na muundo utakaowawezesha wanafunzi kuwa watumishi wenye manufaa, hapo watakapomaliza masomo yao. Maana lazima wawe watumishi; na watumishi hawana haki zinazozidi mabwana zao. Wana kazi nyingi zaidi; lakini hawawezi wakawa na marupurupu zaidi au haki zaidi. Na mabwana wa watu waliosoma ni wananchi; na lazima iwe hivyo.

                Mimi mwenyewe, kwa kusema maneno kama haya katika Afrika Mashariki, na kwasababu ya kuwataka watu waliosoma watende matendo yanayofanana na mawazo haya, nimepata kulaumiwa kwamba nawaandama wasomi  wenzangu, yaani nimekuwa kama mtu anayetafuta kulisaliti kundi lake. Imesemekana kwamba elimu yangu na hulka yangu vinanitia katika kundi la wasomi. Lakini sasa nimewageuka wasomi wenzangu. Kama hivyo ndivyo, ninachoweza kusema tu ni kwamba dhambi hii siitendi peke yangu maana siku hizi wako watu wengi, waliosoma, ambao mawazo yao yanafanana na yangu.

                Lakini kwa kweli naamini kwamba mashtaka kama hayo wanayafanya wale tu ambao hawaelewi msingi wa maneno niliyokuwa najaribu kuyasema. Nami natumaini kwamba baada ya maneno yangu leo ninyi hamtakuwa na mawazo kama hayo. Ni kweli kwamba nayakataa mawazo ya kusema kuwa wasomi ni watu wa pekee, ambao kuwapo kwao kunawastahilisha haki na tuzo, ambazo watu wengine hawazipati. Lakini nakubali kwamba watu waliosoma wana nafasi maalum katika kazi ya kuendeleza mataifa yetu, na kuendeleza Afrika. Nami naomba kwamba ujuzi wao, na nafasi waliyo nayo ya kujua mengi zaidi, itumike kwa faida ya nchi ambamo sisi sote tunaishi.

                Maana sisi wote tunahusiana, kila mmoja kwa mwenziwe. Wale waliosoma na wale wasiosoma, wote tu raia wa taifa moja, bara moja, na dunia moja. Maisha yetu ya siku zijazo yameunganika kiasi ambacho hayawezi kutenganika, na wale waliosoma zaidi kuliko wengine, watategemea sana wananchi wa mahali pale wanapoishi. Maana mkulima anaweza akajitengenezea maisha yeye mwenyewe: akajilimia chakula chake, akajitengenezea viguo na kijumba chake. Mwenye kusoma hataweza kufanya zaidi ya hapo, na kwa kweli atapata taabu hata kujitegemea kiasi anachojitegemea mkulima.  Na kwa vyovyote vile hataweza kupata nafasi ya kutumia ufundi na uwezo wake bila ya kuwapo wananchi. Kwa hiyo, ni kwa faida yake mwenyewe zaidi kuliko faida ya watu wengine, kwa wale wenye kusoma kutumia ujuzi wao kuongeza afya na manufaa ya wananchi wenzao.

                Kuna jambo la mwisho ninalotaka kulisema. Nimekuwa nikitoa maombi kwa vyuo vikuu vya Afrika, na kwa wanafunzi waliomo katika vyuo vikuu vya Afrika, pamoja na wale wengine wote wanaopata elimu ya juu wawe wazalendo wenye kujitoa kwa nchi zao, na kufanya kazi zao zote ziwe na shabaha ya kuhudumia nchi hizo. Mimi siamini kuwa ombi hilo linapingana na kazi ya vyuo vikuu, ambayo huelezwa kuwa ni kazi ya kuchimba na kutafuta ukweli. Maana naamini kwamba nchi huhudumiwa katika ukweli. Naamini kwamba nchi inataka vyuo vikuu, na wanafunzi na walimu wake, wasimame katika kweli kama wanavyoiona, bila kujali yale yatakayowatokea wao binafsi. Hakuna binadamu asiyekosa, viongozi na wananchi wanaoongozwa pia; inawezekana kwamba sisi tumekosea, ama kwasababu ya kutokujua ama kwasababu ya inda ya watu. Ni sehemu ya kazi ya wale wasiobeba wajibu wa kuendesha mambo siku hata siku kutusaidia na kuwasaidia wananchi kwa ukomo wa uwezo wao. Na kufanya hivyo wakati mwingine hulazimu kusema maneno yasiyowapendeza watu, mradi mnayaamini kuwa ni kweli.

                Lakini mtatambua nimesema kwamba kweli lazima isemwe jinsi ile ile inavyoonekana, bila mtu kujali yatakayomtokea yeye binafsi. Ni kiburi cha ovyo mtu kuropoka yale anayoyaona kuwa ya kweli bila ya kujali matatizo yatakayowapata wananchi. Mtu anayepiga makelele ‘Moto! Moto!’ katika darasa lililojaa watoto anaweza akasababisha vifo vingi zaidi kwa msukumano na wasiwasi kuliko yule ambaye aliuona moto akanyamaza; na kwa vyovyote lazima atasababisha vifo vingi zaidi kuliko yule ambaye atawatoa watoto darasani kwa utaratibu. Maana hakuna hata mmoja wetu anayejua ukweli wote; tunaweza tukagunduasehemu mpya ya ukweli, lakini hatuna haki ya kujidai kwamba tunajua zaidi.

                Lazima vyuo vikuu katika Afrika vijaribu kutatua kwa ukweli matatizo wanayoyachunguza. Lazima wayachambue na kuyaeleza kitaalamu; na kutokana na ujuzi huo washauri jinsi ya kuyatatua. Lakini ukweli maana yake siyo kufanya kazi au kufikiri kana kwamba hapa hakuna binadamu. Kipende kisipende, chuo kikuu ni sehemu ya taifa; wakati wa kuchagua mambo ya kuchunguza, na wakati wa kutatua matatizo yenyewe, ukweli huo lazima ukumbukwe. Hiyo ni sehemu ya ule ukweli ambao chuo kikuu lazima kiutatue.

                Afrika inahitaji ukweli kutoka katika vyuo vyake vikuu. Tunapambana na matatizo mapya, na tunahitaji ujuzi wote unaoweza kupatikana katika kuyatatua. Lakini vile vile vyuo vikuu lazima view vyombo vilivyojitoa kutumikia taifa; vijitoe katika kutafuta maendeleo ya nchi zetu. Lazima vitoe huduma ya kizalendo, na kwasababu hiyo itakuwa huduma ya kweli na ya moyo.

Tags:

Share on Facebook
Share on Twitter
Please reload